Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed S. Magaro ameiongoza timu ya wataalam kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua pamoja na upepo, ambapo tarehe 13.02.2024 walitembelea kata ya Kiongoroni.
Timu hiyo ilipita Shule ya Msingi Ruma, Shule ya Msingi Kiongoroni, Shule ya Msingi Jaja pamoja na Shule ya Msingi Pombwe. Licha ya kuona athari hizo zilizotokana na hali ya mvua lakini timu pia imeona majengo mengi ya taasisi hizo ni chakavu sana. Kisha Mkurugenzi Magaro akatoa pole kwa wote na kuahidi msaada wa haraka ili kufanya marekebisho katika majengo hayo.
Sambamba na hilo pia Mkurugenzi Mtendaji ameagiza uongozi wa Kijiji cha Pombwe kufuata taratibu zote za kutoa eneo ili ijengwe shule mpya kwani eneo la zamani si salama tena kwakuwa mvua zikiwa nyingi maji hufika mpaka kwenye majengo ya shule hiyo na kufanya Wanafunzi washindwe kujifunza vyema.
Aidha Mkurugenzi Magaro alipata wasaa wa kuzungumza na Wananchi pamoja na Viongozi wao wa Vijiji ambapo walieleza changamoto zao ikiwemo kupewa msaada wa chakula mapema kwani hali ya uzalishaji mwaka huu si nzuri kutokana na mvua kuwa nyingi.
Wananchi hao walifurahia sana ujio wa Mkurugenzi na timu yake huku wakikiri kuwa ni muda mrefu umepita kwa uongozi mkubwa namna hiyo kutembelea vijiji hivyo.
Naye Ndg. Magaro alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi/walezi wote wenye watoto ambao umri wao unapaswa kwenda shule wawapeleke kuwaandikisha watoto hao na kuwaomba wazazi wachangie chakula ili watoto waweze kula wakiwa shuleni.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.