ASISITIZA UKUSANYAJI NA USOMAJI WA MAPATO NA MATUMIZI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw. Hemed Magaro, kwa mara ya kwanza amekutana na watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Makatibu Tarafa na Wakuu wa Wakuu wa shule za msingi na sekondari, na Wakuu wa Idara katika kikao kazi ili kupeana dira na kupanga mikakati ya pamoja kwa maendeleo ya kibiti.
Katika kikao kazi hicho ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Bw. Magaro amewaagiza watendaji wa Vijiji na Kata, kukusanya na kusimamia mapato kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuwasomea wananchi taarifa ya mapato na matumizi na kuyabandika kwenye mbao za matangazo kila baada ya miezi mitatu.
" Kuwe na uwazi, kusanyeni mapato na wasomeeni wananchi mapato na matumizi ili waweze kujua fedha za serikali zilizoingia, mapato yaliyokusanywa pamoja na matumizi yake" Alisema Magaro.
Vilevile Mkurugenzi Magaro ameagiza taarifa ya mapato na matumizi kusomwa kila baada ya miezi mitatu yaani kabla ya tarehe 10 ya mwezi unaofuata, sambamba na kuhakikisha kila Kijiji kina account ya Benki ambayo itatumika kuhifadhi fedha zinazokusanywa.
" Watendaji Kata nasisitiza, taarifa ya makusanyo ya mapato ikawe kipaumbele katika mabaraza yenu ya Kata " Alisema Hemed Magaro.
Hata hivyo katika kikao hicho Bw. Magaro amewaagiza Wakuu wa shule, Walimu wa kuu na waratibu wa Elimu Kata kukagua, kusimamia na kudhibiti utoro na mimba shuleni kwani ni chanzo cha kushuka kwa ufaulu katika Wilaya ya Kibiti, ikiwa ni pamoja na kuunda timu ya kiutendaji na kuwapa motisha hususani Walimu wao wanapofanya vizuri.
" Kuweni na mikakati, tafuteni mbinu mbalimbali za ufundishaji zitakazosaidia kupandisha ufaulu kwa wanafunzi" Alisema Bw. Magaro.
Katika kikao hicho Mkurugenzi ameelekeza wasaidizi wake wote aliokutana nao leo, kuhakikisha chakula kinapatikana mashuleni kwa kuwaelimisha wazazi kuona umuhimu huo, kwani chakula kikipatikana kitaleta utulivu kwa wanafunzi na kupandisha ufaulu kwa wanafunzi.
"Suala la upatikanaji wa chakula mashuleni siyo la Walimu pekee ni letu sote tushirikiane, ndiyo maana nimewakutanisha wote hapa”. Alisema Magaro.
Aidha Watendaji Kata na vijiji wametakiwa kuhamasisha kilimo ambacho ni UTI wa mgongo wa mapato ya Wilaya kupitia Kata zao, pia Maafisa maendeleo Kata kusimamia vikundi vinavyokopeshwa na kuhakikisha wanarejesha na kuhamasisha jamii kushiriki katika miradi ya Maendeleo.
Mbali na hayo Mkurugenzi amemuagiza Afisa Utumishi kusimamia watendaji wa Kata na Vijiji kutengeneza mpango kazi wa kila mwezi, miezi 3 , 6 mpaka mwaka ambapo kila baada ya mwezi watendaji hao watasoma taarifa ya utekelezaji utakaoonyesha namna anavyotimiza majukumu yake kwa kusimamia nidhamu (kuheshimiana) kulingana na mipaka ya kazi.
Magaro amekemea pia tabia ya uuzaji holela wa ardhi kwa baadhi ya Watendaji wa Kata na Vijiji huku akiwasisitiza kujipanga vizuri kwenda kusimamia vema uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao unatarajiwa kufanyika mwakani ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka wa uchaguzi 2025.
"Swala la Uchaguzi ni sehemu ya kujitathmini kiutendaji kwa kutatua kero za wananchi katika maeneo yenu na kujenga mazingira mazuri ya kukubalika" Alisema Magaro.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.