Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amezindua zoezi la uandikishaji wa Orodha ya Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji,Vitongoji na Mitaa mwaka 2024 , zoezi ambalo limefanyika leo tarehe 11/10/2024 katika Kitongoji cha Lumiyozi kata ya Kibiti.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Zoezi hilo Kanali Kolombo amewataka wakazi wa Wilaya ya Kibiti kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha hali itakayowapa fursa ya kushiriki zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwezi Novemba mwaka huu.
‘’Nendeni mkajiandikishe ili muweze kutimiza haki yenu ya kikatiba na ya kisheria ili muweze kuchagua viongozi mnaowataka,kutokufanya hivyo kutawanyima fursa ya kushiriki zoezi la kupiga kura hiyo siku ikifika’’
Aidha Kanali Kolombo amesema zoezi hilo kufanyika katika kata ya Lumiyozi ni bahati kwani swala hilo lilikuwa likiombwa na Vituo mbalimbali huku akiwasisitiza wakazi wa Kitongoji hicho kujitokeza kwa wingi hata baada ya siku hii ya leo.
Katika hatua nyingine msimamizi Mkuu wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Hanan Bafagih amesisitiza swala la wanachi kushiriki zoezi hili na amebainisha mikakati mbalimbali ambayo imefanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kuwaeleimisha wananchi ili kushiriki zoezi hilo ambalo limeanza rasmi mapema hii leo.
Zoezi la Uandikishaji wa Orodha ya wapiga kura limeanza leo tarehe 11 mwezi Oktoba na linatarajiwa kufikia tamati tarehe 20 mwezi Oktoba 2024.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.