Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amezindua zoezi la Ugawaji na Upandaji miti wilayani Kibiti, kwa kupanda miti 516 katika shule mpya ya Sekondari ya Chief Hangaya iliyopo katika kitongoji cha Lumiozi kwa kushirikiana na wananchi leo tarehe 27.01.2024.
Akisoma ripoti iliyoandaliwa kwaajili ya shughuli hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Bw. Hamadi Mgaluli amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeotesha jumla ya miche 152,326 kwa mwaka 2023/2024 ambayo wanatarajia kuigawa kwa Wananchi na Taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali.
“Moja ya sababu ya kufanya shughuli hii hapa ni ukosekanaji wa miti ya kutosha kwaajili ya kivuli na kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi ya wanafunzi kusoma, lakini pia kuwafanya wananchi waweze kutambua umuhimu wa usafi na uhifadhi wa Mazingira wakiwa shuleni na hata majumbani mwao.” Alisema Bw. Mgaluli
Aidha, Kanali Kolombo ameshiriki zoezi la usafi wa mazingira unaofanyika kila jumamosi ya mwisho wa mwezi maeneo mbalimbali nchini, ambapo wilayani Kibiti usafi umefanyika katika shule mpya ya Sekondari ya Chief Hangaya.
Kanali kolombo ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha Wazazi na Walezi wote ambao bado hawajawapeleka watoto kuripoti shuleni kufanya hivyo kwani kuanzia Jumatatu tarehe 29.01.2024 hatua kali zitaanza kuchukuliwa dhidi yao kwakuwa wiki 2 alizotoa zimekwisha.
Pichani ni matukio mbalimbali ya zoezi hilo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.