Mnada wa kwanza wa uuzaji wa zao la ufuta Mkoa wa Pwani umefanyika Jumamosi ya tarehe 8.6.2024 baada ya kuahirishwa tarehe 6.6.2024 kutokana na changamoto ya mfumo/mtandao wa soko la bidhaa (TMX) kushindwa kufunguka.
Katika mnada huo jumla ya Tani 3385 zimeuzwa ambapo kilo 1,598,878 ni za Wilaya ya Kibiti pekee. Zao hilo limeuzwa kwa bei ya wastani wa juu wa sh. 3685 katika maghala ya Kibiti na bei ya wastani wa chini wa sh. 3605 katika maghala ya Rufiji na Mkuranga.
Awali siku ya tarehe 6.6.2024 Kanali Kolombo akifungua mnada huo aliwaomba radhi wakulima, wananchi na wazabuni waliojitokeza akiwataka kuwa wavumilivu kutokana na changamoto ya mtandao wa soko la bidhaa TMX kushindwa kufunguka na kusababisha mnada huo kuahirishwa.
Aidha amewataka TMX kuandaa mifumo yao mapema kabla ya siku ya mnada ili kuweza kuepuka kusababisha usumbufu kwa wakulima na wazabuni ambao tayari walikwisha jiandaa kwa kuuza na kununua zao hilo.
Aidha Kanali Kolombo ameishukuru Serikali kwa kuweka utaratibu mzuri wa mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na kuwashukuru wakulima kuuridhia utaratibu huo, kwani ndiyo njia pekee nzuri ya kuuza na kupata malipo kwa wakati bila usumbufu kwa bei zilizoridhiwa kwa pamoja.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.