20.12.2023.
Mnada wa Tano na wa mwisho katika msimu wa korosho mwaka 2023 Mkoa wa Pwani umefanyika leo Wilayani Mkuranga ukiwa na wazabuni watano na kufanikiwa kuuza jumla ya Tani 150,938.
Katika mnada huo korosho za daraja la kwanza zimeuzwa kwa sh 1415 na za daraja la pili kwa sh 1110 baada ya wakulima wote kukubaliana kuuza.
Akizungumza na wakulima waliohudhuria mnada huo, Meneja wa Bodi ya korosho Tawi la Dar re Salaam Bi. Domina Mkangara amesema katika msimu huu changamoto ya hali ya hewa ( mvua) imesababisha kushuka kwa makusanyo ya korosho tofauti na matarajio waliyokuwa wamejiwekea.
"Tulitarajia kuuza Tani 20000, lakini tumeuza Tani 10500 hii yote ni kwasababu makusanyo yakorosho kushuka kutokana na changamoto ya hali ya hewa na kusababisha korosho nyingi kuwa chini ya kiwango". Alisema Bi Domina.
Kwa upande wa korosho zilizokuwa chini ya daraja la pili (reject ) wameweka utaratibu wa kuziuza katika soko la ndani kwa wabanguaji wa ndani kupitia vyama vyao vya ushirika.
"Wabanguaji wa ndani, hii ni fursa kwenu itumieni vizuri, hali ya upatikanaji wa malighafi katika viwanda vyenu ipo wazi." Alisema Bi. Domina.
Vilevile kupitia soko hilo la ndani amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanapeleka korosho hizo kwenye AMCOS zao wakati utaratibu wa kuziuza ukipangwa na kudai kwamba watapewa utaratibu wakati wote kuanzia sasa. Pia amewasisitiza wakulima wote kuendelea kuandaa mashamba kwa ajili ya msimu ujao sambamba na kulima mazao mengine katika kipindi hiki cha mvua.
Aidha Meneja wa Corecu Bw.Hamis Mantawela amesema mpaka wanafika mnada wa mwisho wa msimu wa korosho tayari Shilingi Bilion 20 zimetolewa kwa ajili ya malipo ya wakulima ambao mizigo yao ilipitia CORECU na hakuna anayedai.
Mbali na malipo Mantawela amewataka viongozi wa AMCOS kuruhusu usajili mpya kwa kupokea wanachama na tayari Ofisi ya Mrajisi na Vyama vya Ushirika zinaandaa utaratibu wa kusajili wanachama wapya.
Pia Mantawela amevielekeza vyama vyote vya Msingi kutunza pembejeo zilizosalia kwa ajili ya matumizi ya msimu ujao na kwa yeyote atakayekwenda kinyume na maelekezo hayo Sheria itachukua mkondo wake.
"Pembejeo zote ziko kwenye mfumo, na kila kinachotoka mfumo unaonyesha, chondechonde zitunzeni ni Mali ya Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya korosho Juma Abdallah Kibanyula amewashukuru wakulima wote kuwa na uvumilivu mkubwa katika msimu huu ambao umesuasua kutokana na hali ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Mwisho Wakulima wameishukuru Bodi ya korosho kwa kuwasimamia vizuri ikiwa ni pamoja na usimamizi wa kuanika, kuhifadhi na kuhakikisha korosho zinauzika hasa katika msimu huu ambao umekuwa mgumu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
"Tunawashukuru CORECU, kwa kutusimamia na kutuelekeza wakati wote, kutokana na hali ya hewa hatukutegemea kabisa kuuza korosho zetu, kipindi kilikuwa kigumu, cha kufukuzana na jua na mvua. Kazi ilikuwa ni kuanika na kuanua korosho." Walisema Wakulima.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.