6. 4. 2024.
Mbunge wa Jimbo la kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe amewatembelea na kutoa pole kwa wakazi wa Kibiti ambao wameathiriwa na Mafuriko yaliyosababishwa na maji yanayotiririka kutoka vyanzo mbalimbali vya mto Rufiji kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Mpembenwe ametoa pole hizo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Wakazi wa Mtanga-delta, Kipoka na Usimbe ikiwa ni ziara yake maalum kuweza kujionea hali halisi ya Mafuriko na uharibifu uliotokea.
“poleni sana kwa changamoto ya Mafuriko iliyosababisha uharibifu wa mali zenu ikiwa ni pamoja na mazao" Alisema Mpembenwe.
"Niwaombe tu, kwa kipindi hiki mkahamie maeneo yaliyoinuka, Hali ninayoiona hapa siyo salama kwa uhai wa binadamu, lolote linaweza tokea ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha" Alisema Mpembenwe.
Mbali na hayo, Mhe. Mpembenwe aliwataka wananchi hao kuwa na uvumilivu kwani tayari Serikali imekwishaweka utaratibu mzuri wa kuwashika mkono wahanga wote wa maafa hayo kupitia kitengo cha maafa Ofisi ya Waziri Mkuu.
"Kuna watu watapita na huenda wameshapita kuchukua taarifa zenu ikiwa ni pamoja na kuwaandika majina, msiwapuuze, hizo ni takwimu zinazoandaliwa na misaada itaanza kuingia wakati wowote kuanzia sasa" Alisema Mpembenwe.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Afisa Mazingira Zakayo Gideon amesema kwa tathmini iliyofanyika mpaka sasa Kata Tano zimeathirika ambazo ni Kata ya Mtunda, Msala, Maparoni, Kiongoroni na Mbuchi. Pia amesema kamati ya maafa ngazi ya Wilaya inaendelea kufanya tathmini kila siku kuweza kujua ni namna gani wananchi wameathiriwa na Mafuriko hayo ili kuwa na takwimu sahihi.
Aidha wakazi wa maeneo hayo kwa nyakati tofauti pia wamemshuru Mhe. Mbunge kwa kuwatembelea na kuwapa pole. Kupitia Mafuriko hayo wamesema mbali na kuharibiwa mali zao lakini wanahofu ya kukumbwa na baa la njaa kutokana na mazao mengi kuharibiwa kabisa na maji.
Pia walimshukuru Mbunge kwa jitihada zake za kuwajali wananchi wake, kwani ujumbe aliofika nao umewafariji sana hivyo, wanatarajia kupata ahuheni kupitia misaada itakayoletwa kama alivyowapatia salam za Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. SSH.
Katika ziara hiyo Mhe. Mpembenwe aliambatana na Mwenyekiti wa UWT, Mjumbe wa Halmashauri Kuu UWT, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi, Mjumbe wa Kamati ya Siasa, pamoja na Madiwani wa Kata ya Kiongoroni na Mbuchi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.