Afisa Elimu Msingi Zakayo Mlenduka kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mohamed Mavura akiwa ameambatana na Wataalam mbalimbali wa Wilaya, wamefanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa katika shule ya msingi Kiasi kata ya Msala, vyenye thamani ya sh. 110,000,000.
Katika fedha hizo 100,000,000 ni kutoka Serikali Kuu na 10,000,000 ni fedha za mapato ya ndani ambapo mpaka sasa ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa upo katika hatua ya kupandisha Kuta na vyumba vitatu vipo katika hatua za awali za uchimbaji msingi.
Katika ziara hiyo Mlenduka amewaomba wananchi kuupokea mradi kwa kushiriki na kujitolea ili kuongeza nguvu kazi katika mradi huo Ili kuhakikisha vyumba 5 vya madarasa vinakamilika kwa wakati.
Pia Afisa Elimu amewaomba umoja wa vijana CCM (UVCCM) Wilaya kuweka Kambi Ili kusaidia ujenzi huo na kwa kuunga mkono hilo akaahidi kuchangia Michele kg 50, unga kg 25 na Sukari kg 10 kwa ajili ya chakula Cha wanaojitolea wakati huo huo diwani nae akachangia sh. 20000 kwa ajili ya maharage ili kuhakikisha kazi inafanyika na kukamilika kwa wakati kwani madarasa hayo yanatarajiwa kuanza kutumika mwakani (2023).
Kwa upande wa manunuzi ya vifaa Afisa Manunuzi Rose Kahembe akatoa maelekezo ya namna ya kununua vifaa kama fedha ilivyoainishwa kulingana na bei wakati huohuo Afisa Mapato ya ndani Richard Mwalonde akasisitiza kutunza kumbukumbu ya mapato na matumizi kwa maandishi ili kuepuka mikanganyiko pindi kaguzi za tathmini ya miradi zinapofanyika Ili kuwa na uwiano sahihi wa vifaa vilivyo nunuliwa na fedha zilizotumika. Nae Afisa wa TAKUKURU Ndg Emanuel Fransis akaisihi kamati hiyo kuwa wazalendo na fedha hizo kwani endapo taarifa za ubadhilifu zitabainika hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Vilevile kwa nyakati tofauti Maafisa Maendeleo Geoffrey Haule na Agnes Willa , wameisihi Kamati ya ujenzi Inayoongozwa na Mwalimu Mkuu kuishirikisha jamii ikiwa ni pamoja na Wazee Ili kuweka uwazi wa Miradi hali ambayo itasaidia wananchi kujitolea kwa Imani kubwa.
Akitoa pongezi kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Wataalam kwa namna wanavyopambana kuhakikisha ujenzi wa shule unakamilika kwa wakati Diwani wa Kata hiyo Musa Milanzi ameiomba serikali kusaidia kukamilisha Jengo la kina Mama la kujifungulia Katika Zahanati ya Kiasi ambalo mpaka sasa ujenzi upo Katika hatua ya upandishaji Kuta .
Aidhaa Katika Mkutano huo Afisa Maendeleo Tarafa ya Mbwera Geofrey Haule,akaongoza harambee ya kuendeleza ujenzi wa Jengo la kujifungulia kina Mama ambapo ilipatikana jumla ya sh 245,000 ambapo ahadi ni 185,000 na fedha iliyopatikana papo hapo ni sh 60,000 huku ofisi ya Mkurugenzi mtendaji ikiahidi sh .10,000,000 kwa ajili ya kukamilisha Jengo hilo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.