TASAF YATOA RUZUKU KIBITI
UNICEF YAWASITIRISHA MABINTI KUTOKA KAYA ZA WALENGWA.
TAREHE 6/12/2022, Mfuko wa Hifadhi za Jamii TASAF Wilaya ya Kibiti umetoa ruzuku ya septemba -Oktoba kwenye kaya masikini zilizoainishwa ikiwa ni utaratibu wa Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kuzisaidia kaya zisizojiweza (masikini) kwa kutoa fedha za kijikimu ili kuweza kujikwamua kimaisha .
Ruzuku hiyo ambayo hutolewa kwa mwezi kila baada ya miezi miwili huzigusa kaya masikini kwa sifa za kufanyiwa upembuzi yakinifu kutambua walengwa wenye uhitaji ambapo jumla ya sh 886,275 zimetolewa kwenye kaya 38 katika Kijiji cha Mangombela na sh 1,090,372 katika Kijiji Cha Bungu B ambapo kaya 54 zimepokea fedha hizo kwa kila kaya kulingana na kiwango kilichoainishwa.
Vilevile zoezi liliambatana na kukabidhiwa kwa sh 170,000 katika kila kijiji Kwa ajili ya malipo ya watenda kazi na matumizi ya dharura kama ilivyoelekezwa.
Aidha akikabidhi malipo hayo mwezeshaji wa zoezi hilo Laban Kitule amezieleza kaya hizo kuhakikisha fedha wanazozipata zinatumika kwa umakini na kuhakikisha wanajiwekea akiba Kwa kufanya miradi midogo midogo ya kujiingizia kipato sambamba na kujiunga katika vikundi kwa ajili ya kupata mikopo ya Maendeleo.
Katika hatua nyingine TASAF Kwa msaada wa shirika la watoto Duniani (UNICEF) mwezeshaji Laban Kitule amekabidhi msaada wa taulo za kike za kufua, nguo za ndani, ndoo za kuogea na sabuni za kufulia lengo likiwa ni kuwasitiri watoto wa kike waliopo kwenye kaya za walengwa Kwa kujali afya zao, kuimarisha usafi kwa ujumla na kuwaweka huru darasani wanapokuwa katika siku zao.
Jumla ya watoto 36 wamepokea msaada huo, ambapo 18 wametokea Kijiji cha Mangombela na 18 wanetoka katika Kijiji cha Bungu B Katika Kata ya Bungu.
Mwisho Wananchi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti wamefurahishwa na kushukuru baada ya kupokea msaada huo na kuishukuru Serikali ya awamu ya 6 Kwa namna inavyohakikisha inawafikia na kuwasikiliza wananchi wa tabaka la chini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.