13/01/2023 Kamati ya Ulinzi na Usalama, Idara ya Elimu na Muhandisi wa Wilaya ya kibiti imefanya ziara ya dharula ya kutathmini uharibifu wa majengo ya shule 3 zilizoezuliwa mabati kutokana na mvua kubwa iliyonyesha ikiwa imeambatana na upepo mkali.
Wakiwa katika shule sekondari Mtawanya katika Kata ya Mtawanya, kamati hiyo ikiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya Milongo Sanga wamejionea hali halisi ya uharibifu uliotokea wa kuezuliwa bati katika Jengo jipya la maabara ambalo liko katika hatua ya umaliziaji.
Kwa upande wa shule za msingi katika Kata ya Kibiti Jengo la nyumba ya Mwalimu katika shule ya msingi Kitundu limeezuliwa na kuweka nyufa katika kuta wakati katika shule ya msingi Mwangia siku moja kabla chumba cha darasa la Saba kiliezuliwa bati pia kutokana na mvua hizo zinazoendelea kuonyesha.
Kwa nyakati tofauti Katibu Tawala Sanga ametoa pole kwa shule zote zilizopatwa na changamoto hizo, huku akisisitiza hatua za haraka zichukuliwe kufanya marekebisho ya majengo hayo ili yasiendelee kuharibika ukizingatia ni kipindi cha msimu wa mvua bila kuathiri ratiba za masomo zinazoendelea baada ya shule zote kuwa zimefunguliwa Januari 9.
Akitoa tathmini ya madhara hayo, Mhandisi wa Wilaya Kassim Mponda amesema katika Shule ya sekondari Mtawanya kutahitajika mabati 20 kwa ajili ya marekebisho, jipsam bodi 24,mikanda 5, mbao 30 za 2x2 kwa ajili ya papi, kofia 2, misumari inchi 4 kg 1 Kwa ajili ya kenchi na misumari ya bati kg 1.
Aidha, Mhandisi Mponda amesema, katika shule ya msingi Kitundu kutahitajika mabati 14, mbao18 za 2x2 kwa ajili ya papi, misumari ya kenchi inchi 4 kg 1 na misumari ya mabati kg 1 wakati katika shule ya msingi Mwangia kutahitajika mabati 15, mbao 4 za 2 x 3 kwa ajili ya papi ,misumari ya kenchi inchi 4 kg 1,na misumari ya mabati kg 1.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.