Mwenge wa Uhuru ulioanza kukimbizwa rasmi Mkoa wa Pwani tarehe 29 April 2024 hatimaye Jana tarehe 6 Mei 2024 uliwasili katika Wilaya ya Kibiti na kumulika miradi mbalimbali ya Maendeleo ambayo iliridhiwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa UHURU kitaifa Ndg. Godfrey Mzava ukiwa na kauli mbiu isemayo "Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu"
Akikagua miradi Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Uhuru Kitaifa 2024 ametoa wito kwa jamii kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum na kukemea tabia ya baadhi ya watu kuwabagua na kuwanyanyasa watoto hao kwani nao Wana haki kama watu wengine.
Kiongozi huyo amesema hayo alipokuwa akizindua mradi wa kukabidhi chakula kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya Msingi Kitundu ambayo ni shule pekee inayotoa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum Wilayani humo.
Vilevile Kiongozi huyo amesisitiza utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama ambavyo Ofisi ya Makamu wa Rais inavyoelekeza kupanda miti Milion 1.5 kila mwaka ili kurudisha uoto wa asili ikiwa ni pamoja na shughuli zote za uzalishaji kwa kuzingatia uendelevu na utunzaji wa mazingira. Mzava amesema hayo alipokuwa akikagua mradi wa utunzaji miti katika Shule ya Sekondari Mtawanya.
Akiwa katika mradi wa maji Mjawa kabla ya kuweka jiwe la Msingi Kiongozi huyo alisisitiza umuhimu kuendelea kutumia mfumo wa manunuzi ya Umma Serikalini (NEST) ambao umeonekana kupunguza malalamiko ya wazabuni kwa asilimia kubwa na kuachana na tabia ya kuingia mikataba ya makubaliano mezani.
Aidha alipokuwa akizindua mradi wa lishe Shule ya Msingi Itonga, Mzava ameiagiza Idara ya afya Kitengo cha lishe kutokukaa maofisini na badala yake kuambatana na viongozi katika ziara zao ili waweze kutoa elimu ya lishe kwenye jamii nayo iweze kutambua utaratibu mzuri wa ulaji wa chakula na si kula chochote kile bali wazingatie wanakula nini.
Awali mapema asubuhi akipokea Mwenge wa Uhuru wilayani humo Mkuu wa Wilaya Kanali Joseph Kolombo alisema kuwa Mwenge huo utakimbizwa km 83.7 na kumulika miradi ya maendeleo 15 yenye thamani ya sh. Bil 2.4, hivyo miradi yote iliridhiwa kwa kukaguliwa, kufunguliwa na kuzinduliwa.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.