26.03.2024
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na teknolojia Mhe. Omary Kipanga, amekagua Ujenzi wa majengo 9 ya awamu ya kwanza yenye thamani ya sh. Bil. 1.465 ya Chuo cha VETA Wilayani Kibiti kinachojengwa katika Kata ya Bungu.
Akikagua Ujenzi huo amewaagiza wasimamizi wa Ujenzi huo kuhakikisha wanasimamia kwa umakini mkubwa kwa kufuata maelekezo ya michoro waliyopewa ili majengo hayo yaweze kudumu hata kwa vizazi vijavyo, huku akisisitiza kuhakikisha kasoro zilizoonekana zinarekebishwa haraka kabla ya ujenzi huo kukamilika.
"Tumepewa dhamana na Rais kusimamia Ujenzi huu, ni wajibu wetu kusimamia kikamilifu tuweze kutimiza ndoto ya Rais".
"Kwa yeyote atakayeonekana ana nia ya kukwamisha mradi huu tutamwondoa mara moja" Alisema Mhe. Kipanga.
Licha ya kutoa pongezi kwa Serikali kuona umuhimu wa kujenga chuo hicho Kibiti Msimamizi wa ujenzi kutoka chuo cha maendeleo ya wananchi FDC Bi. Renalda Kyaruzi amesema wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa umeme, mtaalam wa manunuzi, usafiri kutokana na hali ya mvua, uzembe kwa baadhi ya mafundi, hati miliki na kuchelewa kufika kwa baadhi ya vifaa.
Aidha Kanali Joseph Kolombo ameshukuru ujio wa Naibu Waziri na wataalam wake huku akiahidi kusimamia na kufuata maelekezo yaliyotolewa kuhakikisha chuo kinakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Pwani Mwl. Sara Mlaki, amemshukuru Mhe. Rais SSH kwa kuujali Mkoa wa Pwani na Wilaya zake hata kuwapelekea miradi ya maendeleo hususani chuo cha VETA sambamba na pongezi nyingi kwa Naibu Waziri kwa kutenga muda wake kukagua mradi huo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.