Wagombea kumi na moja (11) wa nafasi ya Udiwani wamejitokeza kuchukua fomu za uteuzi katika kata ya Mlanzi, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti. Hatua hii ni kufuatia ratiba ya Uchaguzi mdogo wa Madiwani iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Fomu za Uteuzi zilianza kutolewa tarehe 27 Februari, 2024 hadi 04 Machi, 2024. Leo tarehe 04 Machi, 2024 ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kuchukua na kurudisha fomu hizo, lakini pia ndiyo siku ambayo Uteuzi wa Wagombea umefanyika.
Wagombea waliochukua fomu ni 11, waliorudisha walikuwa 9, Walioteuliwa 8 na ambaye hakuteuliwa ni 1.
Wagombea waliojitokeza na kuchukua fomu ni kutoka Vyama vya: UPDP, UMD, ADC, CCM, UDP, DEMOKRASIA MAKINI, CUF, NRA, ACT-WAZALENDO, AAFP pamoja na ADA-TADEA.
Mpaka kufikia leo tarehe 04 Machi, 2024 wagombea wote waliochukua Fomu walipaswa kurudisha fomu hizo lakini ni wagombea tisa(9) pekee ndiyo waliorudisha fomu hizo.
Wagombea waliorudisha fomu za Uteuzi ni kutoka vyama vya UPDP, UMD, CCM, UDP, DEMOKRASIA MAKINI, CUF, NRA, ACT-WAZALENDO, pamoja na ADA-TADEA.
Wagombea ambao hawakurudisha fomu za Uteuzi ni kutoka vyama vya ADC na AAFP.
Baada ya kupokea na kupitia fomu zote zilizorudishwa wagombea nane (08) waliofanikiwa kuteuliwa. Wagombea hao ni: Mussa Juma Maramuah (UDP), Wazuri Yusuph Mbolembole (UPDP), Mketo Athumani Ally (CCM), Ramadhani Saidi Bambo (Demokrasia Makini), Ramadhani Hamisi Ngatakwa (UMD), Seifu Amiri Mwamba (ACT), Abdallah Hamisi Makitia (CUF) pamoja na Athumani Mzuzuri Sadick (NRA).
Mgombea ambaye hakuteuliwa ni Bakari Adinani Mziwanda kutoka chama cha ADA-TADEA.
Kulingana na ratiba ya Uchaguzi mdogo wa Madiwani, Kampeni za Uchaguzi zitaanza kufanyika kesho tarehe 05 Machi, 2024 mpaka tarehe 19 Machi, 2024 wakati uchaguzi mdogo wa Madiwani unatarajiwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2024 katika Kata 23 za Tanzania bara.
Ewe mwananchi usipoteze nafasi ya kumchagua mgombea unayemtaka, Shiriki kila hatua ya uchaguzi huu kikamilifu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.