Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kibiti Mhe. Juma Ndaruke amefika katika kijiji cha Nyanjati kilichopo Kata ya Mahege ili kusikiliza na kutatua kero za viongozi wa kijiji hicho ambao walisusia shughuli za uongozi kijijini hapo kwa madai ya kuwa nafasi zao za uongozi zimewekwa rehani kwasababu ya kutokukamilika kwa maboma matatu yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.
Viongozi hao walidai kuwa kutokamilika kwa maboma hayo ya muda mrefu kunakwamisha shughuli za maendeleo na pia kupoteza sifa zao za uongozi kwa Wananchi kijijini hapo.
Baada ya kusikiliza madai hayo Mh. Ndaruke amewahakikishia viongozi hao kuwa maboma hayo yatakamilika, kuonyesha kuwa anamaanisha hapohapo amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mh. Kanali Joseph Kolombo kuongea na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ndg. Hemed Magaro kukamilisha maboma hayo matatu haraka iwezekanavyo.
"Mkuu wa Wilaya ni wakati wa wewe kujadiliana na Mkurugenzi kuhakikisha angalau boma moja linakamilika kwa namna yeyote wakati tunasubiri fedha za umaliziaji, Serikali kupitia Halmashauri inawajibu wa kuwaunga mkono wananchi katika ukamilishaji wa maboma hayo" Alisema Mhe. Ndaruke.
Vilevile Mhe. Ndaruke amewapongeza wajumbe wa Kamati ya Kijiji hicho kwa kuwa na usimamizi mzuri wa kujenga majengo imara kwa kutumia nguvu za wananchi.
Akipokea maelekezo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema maelekezo ameyapokea na habari njema ni kwamba, tayari bati 80 zimekwishapatikana kwa ajili ya ukamilishaji wa boma moja kati ya maboma matatu na boma la utawala tayari limeshaingizwa kwenye bajeti.
"Ndg wajumbe naomba muwe na uvumilivu tupo kwenye utaratibu mzuri wa kuhakikisha maboma haya yanakamilika na ndani ya siku tatu kuanzia leo bati 80 zitakabdhiwa hapa kwa ajili ya kuezeka boma moja" Alisema Kolombo
Naye Katibu wa ccm Wilaya ya Kibiti Ndg Zacharia Muhidini amewasisitiza wajumbe wa Kijiji kukabiliana na changamoto zinazowakabili kwa kuhakikisha mwarobaini wa changamoto hizo unapatikana na siyo kuzikimbia changamoto kwa kutaka kujitoa katika nafasi zao.
Vilevile Katibu Muhidini ameiomba Serikali kuhakikisha umaliziaji wa maboma hayo unakamilika kabla ya uchaguzi kuanza huku akisisitiza mazingira ya majengo hayo kusafishwa na kuwa safi wakati wote.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya mahenge Mohamed Hingi amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuwa na mwitikio wa haraka baada ya kupewa taarifa ya wajumbe hao na kutoa maelekezo yenye faraja.
Awali wajumbe hao waligoma kuendelea kushiriki vikao vya aina yeyote kijijini hapo mpaka wajue hatma ya ukamilishaji wa maboma hayo kwani yanafanya waonekane wababaishaji kwenye jamii.
Mwisho Mtendaji wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji na baadhi ya wajumbe hao wamewashukuru viongozi hao kwa kufika huku wakisisitiza ahadi zilizowekwa zikamilike kwa vitendo na si maneno.
Hayo yote yamejiri tarehe 29.01.2024 katika kikao na wajumbe wa Kijiji hicho.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.