16.5.2024.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwaajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko wanaoishi kambini Wilayani humo.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Meneja wa Kanda ya Mashariki Kusini Bi. Lilian Kapakala amesema vifaa walivyoleta ni nguo mchanganyiko mafurushi 11, viatu mchanganyiko begi 1 na shuka kubwa aina ya duveti PC 1.
Akitoa pole kwa waathirika hao Bi. Liliani amesema kwamba Mazingira ni uhai kwa wananchi wote hivyo kuna haja ya jamii kwa ujumla kuhakikisha inapambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha mvua nyingi tofauti na msimu.
Akisisitiza zoezi la upandaji wa miti Meneja huyo amesema inapaswa kuunga mkono kauli ya Rais SSH kama alivyoelekeza kuacha kukata miti hovyo kwa ajili ya nishati ya kupikia kwani itatusaidia kuondokana na changamoto za ukataji wa miti, miti takribani 46000 inayopotea kwa mwaka nchini.
Hakuishia hapo Mwakilishi huyo wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC amesisitiza kuwa kuna kila sababu ya wananchi kuhama kabisa katika maeneo ambayo ni korofi na kwenda kuishi katika maeneo salama ili kuweza kuruhusu maji kupita kwa urahisi katika mkondo wake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wakazi wa Kibiti Kanali Kolombo amewashukuru NEMC kwa kuwaona wanakibiti lakini pamoja na shukrani hizo hakusita kueleza uhitaji walionao wananchi wa kibiti kwa sasa kwani wanaomba kusaidiwa kupata mbegu mbalimbali za muda mfupi ili waweze kupanda mazao kwa ajili ya chakula kwakuwa wanajua itafika wakati misaada hiyo itakoma.
Aidha kuhusu utunzaji wa Mazingira Kanali Kolombo amesema atasimamia kikamilifu kuhakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa na kukua ili kurejesha uoto wa asili.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.