Kaimu mkuu wa wilaya ya kibiti Meja Edward Gowele amepokea msaada wa mabati 200 yenye thamani ya shilingi 10,000,000 kutoka Kwa bank ya NMB Kanda ya Dar es salaam Kwa ajili ya kuezekea shule 3 zilizoezuliwa na kimbunga katika shule ya msingi Mangombela, Mlanzi na Ngondai mwezi machi mwaka huu baada ya upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa kusababisha maafa hayo.
Meja Gowele ameishukuru benki ya NMB na watenda kazi wake kwa msaada walioutoa na kuwapongeza kwa namna walivyokua wepesi kuitikia wito baada ya kupokea taarifa za janga hilo katika shule za msingi na akawataka kuendelea na moyo huo wa kujitoa kwaajili ya jamii.
Vilevile Mkuu wa Wilaya mhe. Gowele amepokea komputa mbili, zitakazogawiwa idara ya utumishi katika halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Rufiji kutoka kwa wafanyakazi wa benki ya NMB ikiwa ni utamaduni wao wa kurudisha na kuithamini jamii kwa michango yao binafsi nje ya ofisi.
Katika tukio hilo Meja Gowele amewataka watoto kusoma kwa bidii na kuepukana na utoro shuleni kwani Elimu ndiyo mtaji mkubwa katika ulimwengu wa sasa,huku akiwataka wazazi kusimamia na kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo sambamba na zoezi la kufungua akaunti katika benki ya NMB kwani ni wadau wakubwa wa serikali na jamii kwa ujumla katika kutoa huduma mbalimbali nchini .
Aidha Afisa Elimu Msingi Zakayo Mlenduka kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Mohamed Mavura ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada walioutoa na kusema kwamba , Halmashauri ya kibiti itatoa mbao na misumari kuezeka nyumba za walimu.
Akikabidhi msaada huo wa mabati 200 meneja wa benki ya NMB Kanda ya Dar es salaam Donatus Richard amesema, swala la Elimu ni kipaumbele katika benki yao,hivyo wametoa mabati hayo kuezeka shule hizo 3 zilizopata changamoto ya kuezuliwa mabati lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wanapata elimu wakiwa salama.
Pia katika hafla hiyo Ndg. Donatus ameeleza kuwa wafanyakazi wa benki ya NMB kanda ya Dar es salaam kwa kuona umuhimu wa kusaidia jamii wamechanga pesa zao binafsi na kununua komputa 24 ambazo zitagawiwa katika Halmashauri za wilaya za dar es salaam na Pwani, wamechangia damu katika benki ya damu na pia wamewalipia matibabu Watoto yatima 100 (NHIF cards), Wamewalipia Watoto walioshindwa kilipiwa gharama za matibabu katika hospitali ya Muhimbili Taasisi ya Jakaya kikwete (JKCI) ikiwa ni sehemu yao ya kuijali jamii wanayoihudumia.
Benki ya NMB imekua na utaratibu wa Kila mwaka kutenga asilimia Moja ya faida wanayoipata maalum Kwa ajili ya kurudisha shukrani kwenye jamii inayowazunguka.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.