11.09.2024.
Katibu Tarafa ya Kibiti Ndg. Salum Mzaganya ametoa rai kwa Taasisi ya PAKAYA Wilaya ya Kibiti kushirikisha Serikali za vijiji husika katika shughuli zote za mradi huo ili waweze kupata taarifa za kinachoendelea na kufanya ujasiliamali kwa weledi zaidi.
Mzaganya amesema hayo katika ukumbi wa Halmashauri hiyo alipokuwa akizindua mradi wa uhifadhi wa mazingira delta ya Rufiji kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo.
Katika uzinduzi huo Ndg. Mzaganya amelipongeza shirika hilo lisilo la kiserikali kwa kujikita na kuanzisha huduma ya utunzaji wa mazingira jambo litakalosaidia kutunza mikoko, lakini pia litasaidia kuhamasisha ufugaji nyuki na uanzishwaji wa utalii mdogo mdogo.
Mbali na hayo Katibu Tarafa huyo amesisitiza zoezi la upandaji wa mikoko kuwa endelevu kwa kuhakikisha kunakuwepo na takwimu sahihi, za miti iliyopo na itakayopandwa ili kutambua idadi ya mikoko iliyopandwa kila baada ya muda Fulani.
Aidha Mwenyekiti wa PAKAYA Mhe. Abdallah Pendekezi amesema uzinduzi huo umelenga kutekeleza mradi wa mazingira upande wa delta ya Rufiji- Kibiti kwa kupanda miti ya mikoko katika maeneo yaliyoathirika pamoja na kutengeneza vituo vidogo vya kuhamasisha na kuendeleza utalii wa kiikolojia.
Licha ya hayo Mhe. Pendekezi amesema uanzishwaji na uendelezaji wa ufugaji wa nyuki pia utafanyika katika baadhi ya vijiji jambo litakavyowezesha wananchi kupata kipato kwa kuanzisha vituo vidogo vidogo vya biashara.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa PAKAYA Bw. Hassan Kisoma amebainiaha kuwa Mradi huo utakapoanza utaweza kuchangia pato la Serikali kwani, wanatarajia kwa kima cha chini utaweza kuzalisha Euro 152,000 kwa mwaka.
Mradi huo unategemewa kutekelezwa katika Kata 5 ambazo ni Kiongoroni, Mbuchi, Maparoni, Msala, Mwambao na Salale.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.