Katika kuhakikisha uhifadhi wa Mazingira unaimarika, Serikali imeendelea kuhamasisha na kuweka juhudi za kuhifadhi maliasili za uoto wa asili kwa kutoa makatazo mbalimbali yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu kwa kuwapa wananchi husika kazi mbadala za kuwaongizia kipato.
Katika kutekeleza hilo Serikali iliweza kutoa mizinga ya nyuki, boti za kisasa za Uvuvi ili kuweza kuinusuru delta ya Rufiji hususani Kibiti ambayo kwa asilimia kubwa huathiriwa na shughuli za binadamu.
Hayo yamebainishwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya Kanali Joseph Kolombo alipokuwa akifungua warsha ya mafunzo ya ufugaji wa nyuki, upandaji wa mikoko na utalii ikolojoa katika ukumbi wa Chama cha walimu ulioandaliwa na PAKAYA.
Mkuu huyo wa Wilaya amewaagiza PAKAYA kuwa na malengo makubwa ambayo yataleta tija kwa kuwa na mikakati madhubuti na kuisimamia itekelezeke kama vile kutambua idadi ya mikoko itakayopandwa kwa mwaka, mizinga mingapi itatolewa sambamba na kuimarisha utalii ikolojoa kwa uchumi.
Aidha, Kanali Kolombo ameyashukuru mashirika mbalimbali ya Mazingira yakiongozwa na PAKAYA kwa namna yanavyopambana kurejesha hali ya uoto wa asili uliokuwepo awali katika Wilaya ya Kibiti.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Mazingira na utamaduni (PAKAYA) Mhe Abdallah Pendekezi amesema dhamira ya PAKAYA ni kuhamasisha uhifadhi shirikishi wa mazingira kwenye jamii
Pia Mhe. Pendekezi amesema katika awamu hii tayari wameshanunua zaidi ya mizinga 20 ambayo wanatarajia kuigawa baada ya zoezi la upandaji mkikoko kukamilika ili waweze kuanza ufugaji wa nyuki.
Nao washiriki wa warsha mwisho wa mafunzo wamesema wamefurahia mafunzo na yamewasaidia kujua vitu vipya kama vile namna ya kupanda mikoko, namna ya kujiongezea kipato kupitia utalii ikolojo, umuhimu wa kutunza Mazingira, namna ya kufuga nyuki na faida zake n.k.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.