Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake kupaza sauti kwa pamoja na kukemea changamoto zinazowakabili wanawake wa Tanzania katika nyanja mbalimbali bila kujali itikadi zao.
Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia hadhara katika sherehe ya kilele cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, iliyofanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Vikevile, katika sherehe hiyo Rais Samia ameahidi kuendelea kutafuta suluhu za changamoto zinazowakabili wanawake kwa kukosa huduma ikiwa ni pamoja na kujenga shule za wasichana za sayansi na vyuo vya ufundi ili kuwainua wanawake katika masuala ya kiteknolojia.
Kwa upande wa miundombinu, Rais Samia amesema Serikali imeweka fedha za kutosha kuwawezesha Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuendeleza miundombinu ya barabara vijijini.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kuimarisha Bandari za Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga, Mtwara na Kigoma ili kuimarisha biashara nchini na ndani ya bara la Afrika kwa ujumla. Pia Mhe. Rais amesema atahakikisha Tanzania inakuwa kinara wa uchumi kwa kumsimamia mwanamke kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazouzwa ndani na nje ya nchi kama ilivyopendekezwa na Jukwaa la usawa wa kijinsia.
Rais Samia pia ameeleza kuwa changamoto za mabadiliko ya tabia nchi zimesababisha kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali kama vile kupanda Kwa bei za vyakula hivyo, Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto hizo kuhakikisha Watanzania wanakuwa katika hali nzuri ya maisha na kuweza kujikimu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.