Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amewaelekeza wajumbe wa Timu za Menejimenti (CMT) za Halmashauri ya wilaya ya Kibiti na Rufiji kuongeza jitihada za utekelezaji majukumu kwa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuleta matokeo yatakayoweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
"Kila mtu atekeleze majukumu yake, tunatakiwa tukusanye mapato mengi zaidi kutoka kwenye vyanzo vyetu ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi, na hilo linawezekana tukiweka malengo yetu vizuri” Alisema Kunenge.
Mhe. Kunenge amezisisitiza timu za Menejimenti za Halmashauri kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa jitihada kubwa na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Maelekezo haya ni sehemu ya kazi zenu za kila siku, muwe na takwimu na mikakati madhubuti ya utendaji kwani maagizo hayo yanatarajia utendaji wa taaluma zenu ( wataalam) kwa kujituma zaidi.
Hayo yamejiri jana tarehe 14.2.2024 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ambapo aliwataka Wakuu wa Mikoa katika maeneo yao kukutana na timu za menejimenti za Halmashauri zao.
Maagizo ya Waziri wa TAMISEMI yameelekeza Wakuu wa Mikoa kufuatilia hali ya vipaumbele katika wakati huu wa maandalizi ya Mpango na bajeti ya Mwaka 2024/2025 vinavyojibu hoja za wananchi, mikakati ya ukusanyaji mapato na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Maagizo mengine yameelekeza halmashauri kutoa taarifa zao za upelekaji fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo, ili usimamizi miradi hiyo ukamilike kwa wakati na kwa kiwango kinachoendana na kiasi cha fedha kilichotolewa, taarifa ya utoaji wa asilimia 10 za mapato ya ndani kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu pamoja na mikakati ya utekelezaji taarifa za hoja za Mdhibiti na Mkagunzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG), za Kamati ya Bunge LAAC na (TAMISEMI).
Aidha wa Wakuu wa Wilaya za kibiti na Rufiji , Mhe. Kanali Joseph Kolombo na Meja Edward Gowele kwa nyakati tofauti walisema wamepokea maagizo yote na kuahidi kuyafanyia kazi kama walivyoelekezwa. Pia Wakuu hao wa Wilaya wamesema hali ya Usalama katika Wilaya zao ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kiuchumi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.