Kwaniaba ya MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph kolombo amefanya ziara ya kutoa maelekezo ya ziara ya Mawaziri baada ya kuazimia upembuzi yakinifu uliofanywa na jopo la Mawaziri 8 katika maeneo ya delta ya Rufiji Wilayani Kibiti, na kubaini uwepo wa shughuli za kibinadamu zinazokinzana na Uhifadhi wa MISITU ya mikoko na utunzanji wa mazingira.
Akizungumza na wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo awali aliwataka wananchi hao, kusikiliza kwa umakini maelekezo yaliyotolewa na Mtaalamu kutoka Ofisiy a Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Felix Nlalio ili waweze kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Akisoma maelekezo hayo Kanali Kolombo Alisema kuwa Moja ya maelekezo yaliyotolewa ni pamoja na kusitishwa kwa Shughuli zote za kilimo katika vijiji vyote vilivyovamia eneo la misitu ya mikoko ili kuruhusu uendelevu wa hifadhi hizo.
Vilevile Mkuu wa Mkoa amezielekeza Halmashauri na wakala wa Misitu Tanzania TFS kuanzisha kamati za vikundi vya Uhifadhi wa Misitu ya mikoko vitakavyojihusisha na utoaji wa elimu ili kuweza kudhibiti uoto wa asili uliopo.
Hata hivyo maelekezo hayakuishia hapo pia Mkuu wa Mkoa amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kupitia mikopo kufanya jitihada za kuiwezesha idara ya uvuvi kuunda vikundi ili Wavuvi wapate zana za kisasa zitakazowasaidia kuvua katika maji ya kina kirefu.
Aidha Idara ya Mifugo na Uvuvi imeelekezwa kuandaa na kusimamia ratiba ya uvuvi wa kamba miti, kwa kuwashirikisha wadau wakiwemo wavuvi wadogo wadogo ambao kiuhalisia ndiyo Wahifadhi wakubwa wa eneo la misitu ya mikoko ambayo ndiyo chanzo cha mazalia ya samaki.
Awali Akisoma maazimio hayo Mhandis Nlalio kutoka mkoani Alisema jopo la Mawaziri baada ya kupokea mapendekezo ya uchunguzi uliofanywa limetoa maazimio manne kama ifuatayo:-
1. Kusitisha shughuli za kilimo katika vijiji vyote vya delta vilivyovamia eneo la misitu ya mikoko ili kuweza kuendeleza Uhifadhi huo.
2. Kuanzisha kamati ya vikundi vitakavyokuwa vikitoa elimu ya Uhifadhi wa Misitu ya mikoko. (VNR na BMU) n.k.
3.Wavuvi kuwezeshwa kupata zana zinazokubalika na kuweza kuvua katika maji ya kina kirefu, ili kuweza kupunguza nguvu kwenye maji mafu ambayo ndiyo mazalia ya samaki.
4. Ratiba ya uvuvi wa kamba miti iandaliwe kwa kushirikisha Wadau ambao ni wavuvi wadogo wadogo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.