Baada ya kukosekana kwa Baraza la ardhi na nyumba kwa muda mrefu Wilaya ya Kibiti hatimaye jana tarehe 27.03. 2024 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge akiwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo amewaapisha wajumbe wawili wa Baraza hilo ambao wanakwenda kuanza majukumu yao kuanzia sasa. Walioapishwa ni Ndg. Salum Mkeyenge na Bi. Mariam Sinahofu wote wakiwa ni wakazi wa Kibiti.
Mara baada ya kufanyika uapisho huo mbali na pongezi kwa wajumbe hao Mhe. Kunenge amewataka wakafanye kazi kwa nguvu zao zote kadri ya uwezo wao kwa kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi kwani hakuna aliye juu ya sheria.
"Uteuzi huu umefanyika kwa mujibu wa Sheria, mmeaminiwa na kuteuliwa kuwahudumia wananchi, kafanyeni kazi" Alisema Kunenge.
Vilevile Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa kupatikana kwa Baraza la ardhi na nyumba Wilaya ya Kibiti ni matarajio yake migogoro ya ardhi itapungua ama kutokomezwa kabisa huku akisisitiza Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha hakuibuliwi migogoro mipya.
"Mkurugenzi simamia isizalishwe migogoro mipya, ni matarajio yangu tunakwenda kupunguza na kumaliza changamoto hii" Alisema Kunenge.
Hata hivyo Mhe. Kunenge amesema kupatikana kwa Baraza hilo Wilaya ya Kibiti, sasa linakwenda kufanya Wilaya zote za Mkoa wa Pwani kuwa na mabaraza hayo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango wa Serikali kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na mabaraza ya ardhi na nyumba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema kuanzishwa kwa Baraza la ardhi na nyumba katika Wilaya yake ni faraja kubwa kwani sasa kesi zote zitatatuliwa ndani ya Wilaya na walengwa kupata haki zao bila kutumia gharama kubwa ambapo awali walilazimika kusafiri kwenda Wilaya jirani ya Mkuranga kupata huduma hiyo.
"Nimefarijika sana Baraza hili kuanzishwa Kibiti, sasa wananchi wangu watapumzika na safari na gharama walizokuwa wanatumia kwenda kutafuta haki zao Mkuranga". Alisema Kanali Kolombo.
Aidha Msajili msaidizi wa mabaraza ya ardhi na nyumba Mhe. Mwendwa Mgulambwa ameeleza kuwa moja ya kazi kubwa ambazo wajumbe hao watafanya ni kutoa huduma ya kusikiliza, kushauri na kutatua migogoro yote ya ardhi Wilayani Kibiti.
Naye Mkuu wa kitengo cha Sheria wa Mkoa Mhe. Marcelin Ndimbwa amesema, kutokana na migogoro ya ardhi iliyopo, kuapishwa kwa wajumbe hao ni muhimu katika jamii na wanakwenda kumsaidia Mkuu wa Mkoa majukumu aliyopewa na Mhe. Rais. wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. SSH.
Wateule walioapishwa leo Ndg. Salum Mkeyenge na Bi. Mariam Sinahofu wamesema wameshukuru kwa kuaminiwa na kuteuliwa hatimaye Leo kuapishwa hivyo watasimamia vyema na kuhakikisha haki inatendeka. Pia wamesisitiza kuwa wapo tayari kusikiliza wananchi kwa weledi mkubwa ili kuweza kutambua chanzo cha matatizo na kwa nafasi zao waweze kushauri na kutoa maamuzi kwa haki zinazostahiki.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.