KATIBU TAWALA AONGOZA ZOEZI LA USAFI WA MAZINGIRA, KUPANDA MITI NA KUWEKA JIWE LA MSINGI.
24/4/2023
Ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kilele cha kumbukizi ya sherehe ya Muungano wa Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) Katibu Tawala Milongo Sanga kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo, Watumishi wa Halmashauri na Taasisi wameshiriki kwa kufanya Shughuli mbalimbali za kijamii katika kituo cha Afya kibiti sambamba na kuweka jiwe la msingi Jengo jipya la upasuaji katika kituo hicho.
Haya yamefanyika ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo ameelekeza kufanyika shughuli za kijamii kama vile usafi wa mazingira baada ya kuahirisha Shughuli za gwaride la miaka 59 ya Muungano ikiwa ni mara ya pili mfululizo tangu aingie madarakani.
Wakiwa katika kituo hicho cha Afya, Katibu Tawala Milongo Sanga ameongoza zoezi la shughuli za kijamii kwa kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti na kuweka jiwe la msingi katika Jengo jipya la upasuaji.
Akiweka jiwe la msingi katika Jengo jipya la upasuaji kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Sanga amewataka wasimamizi wa mradi na mafundi kuhakikisha wanatekeleza maelekezo na kukamilisha mradi huo kwa wakati ili Jengo lianze kutumika na kutoa huduma kwa wananchi.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo jipya la upasuaji Kituo cha Afya Kibiti kwa ufadhili wa shirika la KOFIH, lenye thamani ya sh.124,500,000. Mganga Mfawidhi wa Wilaya Dkt.Yohana Kachule amesema, kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza wigo wa utoaji wa huduma za Afya kwa wakazi wa Wilaya ya Kibiti na maeneo ya jirani.
Vilevile Dkt. Kachule amesema, mpaka sasa ujenzi wa jengo hilo upo katika hatua za umaliziaji ambapo kazi zinazoendelea ni kufunga mfumo wa umeme, mfumo wa maji na ujenzi wa njia ya kutembelea (Walk ways) ili kuunganisha Jengo hilo na wodi ya wazazi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.