8.3.2024.
Wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti wameungana na Wanawake wengine duniani kote kusheherekea siku ya wanawake Duniani ambayo huadhimisha kila mwaka ifikapo Machi 8.
Maadhimisho hayo ni mahususi kwa kutoa hamasa kwa Wanawake kuweza kijitathmini kimaendeleo katika ngazi ya uchumi, Siasa na kiutamaduni ili kuleta chachu ya usawa wa kijinsia pia kujitafakari mahali walipotoka , walipo sasa na wanapoelekea.
Akisoma risala mbele ya Mgeni rasmi Afisa Maendeleo ya jamii Irene Urasa amesema kupitia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo " Wekeza kwa mwanamke, kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii" imelenga kuhamasisha jamii kuwekeza kwa mwanamke zaidi kwani mwanamke ni Mlezi na mzalishaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na akikwamuliwa mmoja ni sawa na kuwezesha Taifa zima.
Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali Bado kuna changamoto mbalimbali Wilayani Kibiti zinazoendelea kuwakabili wanawake ikiwa ni pamoja na mfumo dume, kutothamini mchango wa mwanamke kwa baadhi ya wanajamii na kushindwa kujikwamua kutokana na ukosefu wa mitaji.
Hata hivyo Bi Urasa amesema kutokana na changamoto hizo wanapendekeza jamii kuelimishwa kutambua mchango wa wanawake, faida za kuwekeza na hasara ya kutowekeza kwa wanawake.
Historia inaonyesha maadhimisho hayo yalitokana na jitihada za wanawake 15,000 ambao waliandamana mjini New York huko nchini Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kazi, kupatiwa ujira wa kuridhisha na kupata haki ya kupiga kura.
Kabla ya Mgeni rasmi kuongea na halaiki ya wanawake waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo, Diwani wa Maparoni mhe. Bakari Mpate kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri amesema Baraza la Wahe. Madiwani Wilaya ya Kibiti linapambana na litaendelea kupambana kuhakikisha 10% ya mapato ya ndani inawafikia wanawake, vijana na walemavu kwa kutoa mikopo kama ilivyoelekezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akimwakilisha Mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala Ndg. Salim Malogwa amesema jamii inapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali kuweza kusaidia upatikanaji wa haki za Msingi za Wanawake bila kujali hali zao ili kuweze kuleta maendeleo chanya katika uchumi na Ustawi wa Jamii.
Hata hivyo amesisitiza kuwa katika kuhakikisha kuwa haki hizo zinapatikana ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanawake wanawezeshwa zaidi na kuwa sehemu ya ushindani katika uchumi wa Teknolojia ili waweze kushiriki katika shughuli za maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Mwisho Bw. Malogwa amesisitiza wanawake kutumia Teknolojia kwa mtazamo chanya ili waweze kupiga hatua zaidi katika masuala mbalimbali hususani katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.