Tarehe 14/02/2023 Taasisi ya Youth Crossing Boundaries Foundation (YCB) yenye ofisi zake Wilaya ya Ubungo kata ya Manzese Jijini Dar es salaam, Ikiongozwa na Mkurugenzi wake Bw. Alphonce Leonard imetembelea shule ya msingi Mng’aru iliyopo kata ya Dimani Wilaya ya Kibiti kwa lengo la kuonyesha upendo kwa Wanafunzi 120 wa shule hiyo kwa kuwachangia unga, Rimu papers, vikombe, pamoja na sukari.
Taasisi hiyo inayojihusisha pia na kuwasaidia wanafunzi Mashuleni na hasa masuala yanayohusu afya zao, inatarajia kuingia mkataba na Uongozi wa Shule hiyo ili kuweza kufadhili unga na sukari kwa ajili ya uji wa wanafunzi wa shule hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kama ambavyo walifanya mwaka uliopita katika shule ya msingi Kinyamale iliyopo kata ya Bungu Wilayani Kibiti.
“Leo ikiwa ni siku ya wapendanao tumechagua kuja hapa kuonyesha upendo kwa Watoto hawa, na tumekuja na zawadi kidogo kwa ajili yao ili kuunga jitihada za Mhe. Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia unga ,sukari na vikombe.” Alisema hayo Bw. Alphonce.
Aliendelea kusema “Ikiwa shule itaridhia tutaingia Mkataba wa kuchangia unga na sukari kwa ajili ya uji hivyo tutahitaji kupata bajeti ya mwezi ili kujua gharama za kuhudumia kwa mwaka mzima.”
Hatahivyo Mkurugenzi wa Taasisi hiyo alitoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi kuendelea kuchangia huduma za chakula cha mchana shuleni ili kuwajengea wanafunzi uwezo mzuri wa kustahimili masomo yao na kuongeza ufaulu.
Naye Diwani wa kata Hiyo Mhe. Yusuph Mbinda, alieleza kuwa wanafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha agizo linatekelezwa na chakula kinapatikana shuleni siku zote wanafunzi wawapo shuleni.
“ Sisi kama Kijiji hatujakaa kimya juu ya suala hili hivyo katika kuunga juhudi za Mhe. Rais, tumesafisha shamba lenye ukubwa wa ekari 3 kwa ajili ya kupanda ufuta wa shule utakao saidia ununuzi wa Chakula baada ya mavuno. Hivyo tunategemea suala la njaa kwa wanafunzi wetu shuleni litakuwa historia ” alisema Diwani.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.