Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16.6 ikiwa ni kumbukizi muhimu kwa ajili ya watoto wa Kitongoji cha Soweto nchini Afika Kusini waliouawa kutokana na ubaguzi wa rangi. Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kibinadamu ikiwemo kutobaguliwa na haki ya kupata elimu bora hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi. Kutokana na tukio hilo uliokuwa umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) uliazimia kuwa tarehe hii kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeungana na nchi nyingine za Afrika kuadhimisha siku hiyo katika viwanja vya shule ya Msingi jaribu mpakani, sherehe ambayo ilipambwa kwa burudani mbalimbali kutoka kwa watoto kama vile kwaya, igizo, shairi, ngoma n.k zenye jumbe muhimu kuhusu watoto ikiwa ni pamoja na kupewa haki zao za msingi.
Siku ya mtoto wa Afrika Mwaka 2024 imebeba kaulimbiu yenye ujumbe maalum usemao "ELIMU JUMUISHI KWA WATOTO IZINGATIE MAARIFA,MAADILI NA STADI ZA KAZI".
Katika maadhimisho hayo Mgeni rasmi Katibu Tarafa wa Kibiti Ndg. Salum Mzaganya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo amesema, Mkuu huyo amewaagiza wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao katika maadili, kuwalinda na kuwapatia mahitaji yao ya Msingi. Pia ameiagiza Taasisi zinazohusiana na ulinzi wa watoto kuchukua hatua kali kudhibiti matukio sambamba na jamii kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki za watoto kama vile ubakaji, ulawiti n.k. pia Mkurugenzi Mtendaji kuwa na bajeti kwa ajili ya shughuli za ulinzi wa mtoto.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro alisema, kutokomeza ukatili kwa watoto si suala la mtu binafsi bali ni jukumu la jamii nzima kwa ujumla kusimamia malezi ya watoto hao.
Aidha katika risala ya watoto hao waliohudhuria ilieleza kuwa watoto wamependekeza wazazi na walezi kuelekezwa namna ya kutimiza wajibu wao, kuchukua hatua kali kwa wanaowafanyia ukatili, elimu ya ukatili na lishe kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na Serikali kuweka Mazingira rafiki katika shule na kusimamia upatikanaji wa chakula mashuleni.
Mwisho katika sherehe hiyo Taasisi ya Kalamu Education Foundation na CAMFED walitoa zawadi za vifaa mbalimbali kwa watoto walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano, taulo za kike kwa mabinti pamoja na sabuni ya unga ya kufulia.
Wageni mbalimbali walihudhuria sherehe hiyo wakiwemo wale kutoka Taasisi ya kidini ya KKKT Dayosisi ya Pwani na Mashariki, pamoja Paralegal kutoka Ilala na Kinondoni.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.