Tarehe 7.3.2023
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeungana na nchi nyingine ulimwenguni kusheherekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika uwanja Samora Wilayani humo na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, Chama, Taasisi na wananchi mbalimbali bila kuwasahau Wanafunzi.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yalianza kuadhimishwa kuanzia tarehe 02/03/2023 na kufikia kilele tarehe 08/03/2023 kwa kunogeshwa na Kauli mbiu ya mwaka huu ni isemayo “UBUNIFU WA MABADILIKO YA TEKNOLOGIA NI CHACHU KATIKA KULETA USAWA WA KIJINSIA”.
Historia ya maadhimisho haya ni matokeo ya vuguvugu la wafanyakazi wanawake elfu kumi na tano walioandamana mwaka 1908 jijini New York Marekani wakidai kupewa muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura ambapo wazo la siku hii lilitolewa mwaka 1910 na mwanaharakati wa kikomunist mtetezi wa haki za wanawake Bi Clara Zetkin.
Katika maadhimisho hayo yaliyoanza kwa maandamano na kupokelewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mhe. Ramadhan Mpendu mbaye alikuwa ndiye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amesema, kuwawezesha wanawake kuingia katika Viwanda vidogo vidogo kunaongeza ubunifu kwenye Shughuli wanazofanya kulingana na mabadiliko ya teknologia.
Vilevile Mhe. Mpendu amesema, wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya familia na Taifa Kwa ujumla, hivyo bado tunajukumu kubwa kama Serikali la kuelimisha jamii kutambua, kuheshimu na kuthamini suala la USAWA.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa, kuwawezesha wanawake kuwa na mazingira mazuri ya kisheria kutasaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika kaya mbalimbali nchini, huku akizikumbusha jamii kutambua na kujua umuhimu wa kuwawezesha wanawake, kushiriki katika michakato ya Shughuli za maendeleo ili kuleta maendeleo chanya Kwa wananchi kiuchumi na kijamii kwa ujumla.
“Wanawake ni watu muhimu sana katika jamii, wapewe kipaumbele katika kuwawezesha kielimu, kiuchumi, kisiasa na kijamii” Alisema Mpendu.
Aidha ili kuleta MABADILIKO ya maendeleo kibiti Mpendu ambaye pia ni Diwani wa Bungu, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, jambo litakalo wasaidia kupanuka kimawazo na kupata haki zao za Msingi.
Katika sherehe hiyo Katibu wa chama cha Walimu Mwl. Crecencia Tindwa amewataka wazazi kuwa na tabia ya kufuatilia mwenendo wa watoto katika masomo yao ikiwa ni pamoja na kukagua madaftari yao, huku akiwasisitiza wanawake kupendana, kujiendeleza kielimu na kujifunza vitu vipya na vizuri kutoka kwa wengine.
Vilevile Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake Wilaya ya Kibiti Latifa Augustino amewasihi wanawake kufanya kazi Kwa bidii, kujituma na kuwa na tabia ya kuweka akiba sambamba na kuwekeza kwa manufaa ya baadaye. Pia afisa ustawi wa jamii Ansila akatoa elimu ya malezi Bora ya watoto wao na kuwapa huduma muhimu wakati Patricia Mdemu kutoka NGO’s ya Jicho angavu na msaada wa kisheria akitoa elimu juu ya ndoa na haki zake za msingi.
Naye mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibiti bi Tatu mkumba katika maadhimisho hayo ameitaka Jamii kupinga ukatili wa kikinsia kwa nguvu zote Wakati Diwani wa Kata ya Kibiti Mhe. Hamidu Ungando Yeye amesema kuna kila sababu ya kusimamia ustawi wa kina mama waweze kujikwamua kwani kina mama ni viongozi.
Awali mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi Raya Mlawa mwandishi wa vikao (CC) wa Halmashauri ya kibiti alisema shughuli zilizofanyika katika kuadhimisha ni pamoja na kufanya usafi katika kituo cha Afya kibiti , kuwafariji wagonjwa katika wodi ya wanawake, watoto na wanaume na kutoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wa kike waliofanya vizuri shule ya sekondari Mjawa.
Pia sherehe hiyo ilitumbuizwa kwa kufanya maonesho ya shughuli za vikundi vya ujasiriamali, kupima uzito na kupewa ushauri na kufanya igizo la rushwa ya ngono makazini lililoshirikisha ushiriki wa Taasisi ya kupambana na Rushwa TAKUKURU.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.