7.2.2023
Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kwa kushirikiana na shirika la Chuo Kikuu cha Johns Hopkings kupitia mradi wa Breakthrough Action wamefanya Tamasha kubwa la kuhamasisha jamii kwa kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo mbalimbali katika viunga vya stendi ya mabasi Kibiti tarehe 7 Februari, 2024.
Licha ya kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa chanjo na uchanjaji wa chanjo za aina mbalimbali pia wameendesha zoezi la vipimo vya magonjwa mbalimbali kama vile malaria Upungufu wa Kinga Mwilini/ UKIMWI pamoja na kuchangia damu.
Katika Tamasha hilo Taasisi hiyo imetumia jukwaa la Mashindano ya nusu fainali ya kombe la Afrika (AFCON) kuelimisha Jamii hususani kwa kuwalenga wanaume kuweza kujua zaidi umuhimu wa chanjo.
Kauli mbiu ya Tamasha hilo imevinjari na kibwagizo kisemacho " kuwa bingwa ambaye familia yako inahitaji" Chanjo ni Afya, Onesha Upendo pata chanjo na mpeleke mtoto akachanjwe .
Wakitoa utambulisho wa ugeni huo, Katibu Tawala wa Wilaya , Mkurugenzi Mtendaji na Mganga Mkuu, kwa nyakati tofauti wameipongeza Taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu ya chanjo huku wakiwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo kupima ,kuchanja na kuchangia damu.
"Leo tumepata ugeni mkubwa, ndg Wananchi jitokezeni kwa wingi kutumia fursa hii njooni mpate chanjo na mpime Afya zenu" Walisema Viongozi hao.
Akimuwakilisha Mgeni rasmi Dr.Festo Ndugange Naibu Waziri Tamisemi, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema Serikali imekuwa na juhudi kubwa, kuhakikisha inadhibiti magonjwa ya milipuko na yasiyo ya milipuko kwa kutoa chanjo kama vile, Pepopunda, Ndui, Polio, Uviko19 (Korona) n.k.
Kanali Kolombo aliendelea kusema kwamba katika awamu zote za Uongozi wa viongozi Tanzania, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa Afya kutoa huduma kwa kutumia Afua zote kudhibiti na kupunguza vifo kwa wananchi hususani miaka ya 2020 katika mlipuko wa ugonjwa wa “COVID 19” na kazi inaendelea.
Kufuatia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali Kanali Kolombo amewasisitiza Wananchi wa Kibiti kuendelea na utaratibu wa kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, Kula chakula cha moto ili kuweza kujinga na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, Kufanya mazoezi sambamba na kula Lishe Bora kwenye familia.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya na Mgeni rasmi katika Tamasha hilo, amewataka watalaam kuendelea kufanya tafiti nyingi ili kupata chanjo na dawa madhubuti dhidi magonjwa yanayosumbua wananchi kwa wingi kama Malaria, Mfumo wa kupumua, Upungufu wa damu na mengineyo.
Mwisho Kanali Kolombo amempongeza Mhe Rais Dkt. SSH kwa kuona umuhimu wa chanjo nchini huku akiipongeza wizara ya Afya kwa ushirikiano mzuri na wadau jambo ambalo litaendelea kuimarisha huduma na kufikia malengo ya kuwa Taifa lenye Afya Bora.
Nao viongozi wa Chama waliohudhuria Tamasha hilo wamemshukuru Rais Dkt. SSH kwa kufanya kazi kwa karibu na jamii na kuwasogezea huduma ambapo pia wamepata elimu. Kupitia mashindano hayo ya AFCON Tamasha limewasogeza wanaume wengi kushiriki kwakuwa wanaume hupenda mchezo wa soka.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.