WAJUMBE WAAGIZA KUANZA KUTUMIKA KWA SOKO HILO
Wajumbe wa Kamati ya Taifa Uongozi ya TASAF wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua soko la Bungu lenye thamani ya sh.65,261,175. ambapo limejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kuchangia kiasi cha sh 8,220,950 huku TASAF ikichangia sh 57, 040, 225.
Akizungumza na hadhara pamoja na wanufaika wa TASAF waliojitokeza Mhandisi Rogatus Mativila Mjumbe wa Kamati ya Uongozi TASAF ( Naibu Katibu Mkuu Miundombinu TAMISEMI) amewataka wananchi kuhamia na kuanza kutumia soko la bungu huku akiwaondoa hofu kuwa, hakuna huduma ambayo iko mbali, bidhaa ikiwa sokoni wateja huifuata ilipo.
" Ndg niwatie moyo, fanyeni biashara katika soko hili, na mradi huu hatukuuleta kwa bahati mbaya, tulizingatia na kutekeleza maombi yenu" Alisema Mhandisi Mativila.
Vile vile Mhandisi Mativila amesema, kujengwa kwa soko halafu lisitumike ni uharibifu wa rasilimali fedha kwani fedha hizo hutafutwa kwa nguvu kubwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, hivyo ni vema kuzitendea haki fedha zinazotolewa na Mhe.Rais.
"Tuko hapa kutembelea miradi ya Maendeleo inayofadhiliwa na TASAF, tujionee uhalisia wa namna fedha zilivyotumika" Alisema Mhandisi Mativila.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa soko hilo ambalo kwa sasa linatumiwa na idara ya Mahakama, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bungu A Sultan Musa Kwangale amesema, baada ya soko hilo kukamilika liliweza kutumika kwa muda wa miezi 5 pekee na wananchi kuhama kwa madai kwamba soko liko mbali.
Hata hivyo Kwangale amesema tayari wananchi wamekwisha hamasishwa na wameridhia kurejea katika soko hilo wanatarajiwa kuanza kutoa huduma sokoni hapo mapema baada ya Mahakama kukabidhi soko hilo ifikapo 7.8.2023 mwaka huu.
Kwa niaba ya wananchi baada ya kuridhia kufanya shughuli zao katika soko la TaSAF Kwangale amesema wanaomba Serikali iwasaidie kiasi cha fedha kuweza kufanyiwa ukarabati sokoni hapo ikiwa ni pamoja na mabati, kupaka rangi, miundombinu ya maji na choo.
Akiwakaribisha Wajumbe wa TASAF Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo aliishukuru Serikali ya awamu ya 6 kupitia TASAF kwa namna inavyohakikisha wananchi wake wanapata maendeleo, huku akiwataka wananchi kusikiliza kwa makini ugeni huo na kufuata maelekezo.
"Nafurahishwa sana na maendeleo yanayofanywa na TASAF, tuwaunge mkono, tusiwakatishe tamaa" Alisema Kolombo.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibiti Ndg, Zacharia Yahya Muhidini, ameishukuru TASAF kwa kazi nzuri wanazofanya huku akiwasihi kuikumbuka kibiti katika bajeti ijayo, kwani bado kuna walengwa ambao ni wahitaji.
Mwisho Diwani wa Bungu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu, ameishukuru TASAF kwa kuona umuhimu wa kuufatilia mradi huo na kuishukuru Serikali kwa kuwajali Wananchi wa kibiti na Tanzania kwa ujumla.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.