Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Health Promotion Support (THPS) ambalo linasaidia Serikali ya Tanzania kutoa huduma za kiafya kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wake wa kupambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa makundi maalumu na yaliyo katika hatari zaidi katika jamii, limetoa baiskeli 13 kwa watoa huduma wa Kibiti ili ziweze kuwasaidia kufanya shughuli za Ukimwi jamii.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana amewataka watoa huduma hao kwenda kutumia baiskeli hizo kwa kazi iliyokusudiwa na kwa kuwa kazi hiyo ni ya kitaaluma anaamini THPS wamekwishawawezesha watoa huduma namna ya kuwahudumia wanajamii.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mwl. Zakayo Mlenduka amelishukuru shirika hilo kwa usaidizi walioutoa kwani wameona ipo haja ya kuwafikia wanajamii huko walipo.
“Niwaombe ninyi mnaokwenda kuvitumia vifaa hivi vikatumike kwa kazi iliyokusudiwa, watu wakafikiwe, wakajengewe uwezo na uelewa hususani matumizi sahihi ya ARV’s na kuhamasisha watu wakapime ili ikiwa watagundulika kuwa na maambukizi basi waanze kutumia dawa mapema mwisho tukawe na jamii isiyo na maambukizi” Alisema Bw. Mlenduka.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.