Wakati jengo la Ofisi ya kituo cha mkongo wa Taifa wa mawasiliano Wilaya ya Kibiti likiwa imekamilika kwa 95% Viongozi wa Kampuni ya simu Tanzania TTCL wamewasili wilayani humo kwa lengo la kutoa uelewa juu ya matumizi ya mkongo huo unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi mei mwaka huu baada ya ujenzi huo kukamilika.
Akizungumza na Kamati ya ulinzi na Usalama pamoja na Wakuu wa Idara na vitengo Afisa Mkuu Ofisi ya mkongo wa Taifa makao makuu Bw. Edson Richard amesema, wamefika Kibiti kwa lengo la kutoa uelewa kwa sababu wameongeza njia za mkongo ambapo awali Wilaya ya Kibiti haikupitiwa na mkongo huo.
Vilevile ndg Richard amesema, Serikali imejenga mkongo wa Taifa kwa madhumuni makubwa ya kujenga uchumi na jamii habari (information society) ambao kazi yake kubwa ni kusafirisha mawasiliano yote nchini kama vile, maongezi ya simu, huduma ya internet, taarifa mbalimbali za ujumbe mfupi (sms), huduma za kifedha kama vile kutuma na kupokea pesa kwenye simu (mobile transfer money), radio na television sambamba na kuwezesha ufanisi wa huduma za mawasiliano kwenye Taasisi za fedha (bank na ATM).
Naye Meneja wa huduma kwa wateja TTCL Bi. Wendlyne Mbagga amesema, kupitia makampuni yaliyosajiliwa kutoa huduma za simu na internet miundombinu ya mkongo wa Taifa wa mawasiliano utatumika kutoa huduma za kisasa za utumaji na upokeaji wa taarifa pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma za Afya mtandao (e - health), elimu mtandao ( e - learning), kilimo mtandao ( e - agriculture) Serikali mtandao( e - government) n. K.
Aidha Bi. Wendlyne amesema kupitia huduma hizo wananchi katika maeneo mbalimbali watafaidika kwa sababu huduma za mawasiliano zitaimarika, ajira zitaongezeka na vipato vitaongezeka kwani kutafanyika biashara kama vile m pesa, tigo pesa, mawakala wa mabenki mbalimbali n.k
Mara baada ya kupokea ugeni huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameishukuru kampuni ya simu ya TTCL kwa ujio wake mzuri, huku akikiri maendeleo ya mawasiliano yanaonekana ukilinganisha na ilivyokuwa awali pamoja na kumpongeza Mhe. Rais Dkt SSH kwa juhudi anazozifanya kuhakikisha kila Mtanzania anapata mawasiliano popote alipo.
Mbali na hayo Kanali Kolombo amesema ujio wa mkongo wa Taifa Wilaya ya Kibiti ni faraja kubwa kwa wakazi wa Kibiti kwani pamoja na uwepo wa mawasiliano kuna baadhi ya maeneo bado yana changamoto, na ni Imani yake kwamba Sasa kero hiyo inakwenda kupata mwarobaini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.