24.04.2024
Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) kupitia Wizara ya Elimu limetoa misaada ya vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni sehemu ya kuwajali wanafunzi waliopatwa na mafuriko katika Wilaya za kibiti na Rufiji.
Awali akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Elimu ya Watu Wazima Tanzania (Mratibu wa majanga Sekta ya Elimu) Dkt. Magreth Matonya ametoa pole kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti kwa kufikwa na madhira hayo ya Mafuriko yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha.
Vifaa vilivyotolewa ni vifaa vya kufundishia kwa walimu, vifaa vya kufundishia Sayansi (science kit), vifaa vya michezo mbalimbali, vifaa vya kufundishia watoto wa Elimu ya Awali, vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi, na mahema makubwa yenye uwezo wa kutengeneza darasa lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 45.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewashukuru UNICEF kupitia wizara ya elimu kwa kuguswa na kuitikia wito kwa haraka baada ya kufikishiwa kilio chetu kutokana na janga hilo la mafuriko.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro kwa niaba ya Baraza la Madiwani na watumishi wote amewashukuru UNICEF kwa msaada waliotoa huku akikiri kuwa msaada huo unakwenda kusaidia watoto wa darasa la nne na la Saba ambao wapo kwenye madarasa ya mitihani.
Misaada hii inakuja ikiwa ni utekelezaji wa ahadi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alipoahidi kuleta msaada wa VIFAA kwa watoto hao wakati Serikali ikiendelea kujipanga na kuhakikisha wanafunzi ambao shule zao zimeathiriwa na mafuriko nchini kote wanaendelea na masomo.
"Mafuriko yasiwe sababu ya mtoto yeyote kukosa Elimu, Shule zilizo karibu ziendelee kuwapokea wanafunzi kutoka shule zilizoathirika na kufungwa kuendelea na masomo huku Serikali ikiendelea na mikakati mingine ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto hiyo, wazazi ruhusuni Watoto wote kwenda shule zilizo karibu na maeneo waliyopo kuendelea na masomo" Alisema.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.