Wizara ya afya Maendeleo ya Jamii Jinsia wazee na watoto kwa kushirikiana na watu wa Marekani,Amref,Mkukuta na TCDC kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu Wilaya ya Kibiti wamefanya zoezi la kupima kifua kikuu kwa x ray na kutoa matibabu kwa waliopatikana kuwa na tatizo bure katika Kijiji cha Nyamisati Kata ya Salale na Jaribu Kata ya Mjawa kwa kutumia gari maalumu lenye maabara ya kisasa linalotoa huduma inayotembea yaani mobile clinic.
Mratibu wa USAID Afya Shirikishi mkoa wa Pwani Bi.Georgia Kasori ambaye amesimamia zoezi hilo amesema,lengo la kutoa huduma hiyo ni kuhakikisha watu wanapewa elimu,wanapima na kupewa matibabu kwa watakaopatikana na tatizo ikiwa ni pamoja na kuwapa afueni kwa gharama za vipimo vinavyotakiwa kupima ugonjwa huo kama vile x-ray,kwani katika hali ya kawaida gharama zake huwa kubwa.
Vilevile Bi Kasori ameitaka jamii kujitokeza na kuwa na tabia ya kupima na kujua afya zao ili watakaopatikana na ugonjwa kuanza matibabu mapema,wakati huo huo akawapongeza wananchi wa vijiji hivyo Kwa namna walivyojitokeza kupima na kujua afya zao.
Akitoa takwimu za mahudhurio ya zoezi hilo Bi Kasori amesema jumla ya watu 350 wamejitokeza kuhojiwa na kupimwa ,waliopigwa X-ray ni 316 ambapo wanaume walikua ni 105 na wanawake walikuwa 211,na waliogundulika kuwa na tatizo na kuanzishiwa matibabu walikuwa 86.
Bi Kasori amebainisha kwamba Katika siku ya kwanza wakiwa Katika kata ya salale Kijiji cha Nyamisati jumla ya watu 200 walihojiwa na kupewa Elimu,176 kati yao walipiga x-ray , wanaume ni 92 na wanawake ni 84 na 43 kati ya waliopigwa X-ray walipatikana na tatizo na kuanza matibabu.
Katika siku ya pili wakiwa Katika kata ya Mjawa Kijiji cha Jaribu jumla ya watu 150 walihojiwa na kupewa elimu,140 walipiga x-ray,23 kati yao waligundulika kuwa na tatizo na kuanza matibabu ,kati yao wanaume ni 13 na wanawake ni 10 .
Mbali na upimaji wa kifua kikuu pia kulifanyika zoezi la kupima virusi vya ukimwi (VVU),kupima uviko 19 (corona) kutoa elimu ya lishe na uhamasishaji wa matumizi ya bima ya afya iliyoboreshwa na inayopatikana bei nafuu(ICHF).
Kwa upande wa zoezi la kupima vvu waliopimwa ni 67 na waliofahamika kuwa na tatizo na kuanzishiwa dawa ni 4, wakati waliopewa chanjo ya uviko ni 72 ambapo kati yao wanaume ni 31 na wanawake ni 41.
Aidha Mratibu wa kifua kikuu Wilaya ya Kibiti Dr.Stanley Alfred amepongeza idadi ya watu iliyojitokeza kupima na kuanza matibabu kwa waliojulikana wanachangamoto na walichagua maeneo hayo kwa makusudi ili wale ambao hawakupata huduma kipindi kilichopita wapate huduma karibu kwani wengi wao hushindwa kufika wilayani kupata huduma hiyo kutokana na umbali. Pia ameisihi jamii kuwahi kituo cha Afya mapema kupata huduma pale wanapohisi wana dalili moja wapo ya ugonjwa kwani kifua kikuu kinatibika.
Naye mratibu wa bima ya afya iliyoboreshwa (ICHF) Wilaya ya Kibiti Ansila Lugongo akatoa elimu juu ya bima na kusema kwamba bima hiyo ni nafuu na rahisi kwani hupatikana kwa sh 30,000 kwa mwaka huku ikiweza kuhudumia watu 6 katika Kila kaya na kuweza kutibiwa katika hospitali zote za mkoa wa Pwani. Bi. Ansila ameisisitiza jamii kukata bima kwasababu faida ya bima hiyo ni pamoja na kupata huduma za matibabu kama kipimo cha Ultra sound,upasuaji mdogo,kulazwa ,kupata rufaa ya kwenda hospital nyingine.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.