10.09.2024.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ametoa siku mbili kwa Mamlaka ya bandari na TEMESA kumpelekea taarifa ya kujieleza kuhusu chanzo kilichosababisha usafiri wa meli kukwama kutoka bandari ya Nyamisati kuelekea Mafia kwa siku nzima.
“Ninawapa siku mbili tarehe 12.09.2024 nahitaji kupokea taarifa ya kujieleza nijue sababu ya changamoto hii" Alisema kolombo.
Kanali Kolombo amesema hayo alipokuwa akizungumza na abiria waliokwama katika bandari ya Nyamisati ambao walikuwa wakielekea Mafia.
Akiwa katika jengo la kupumzikia abiria katika Kijiji cha Nyamisati Kanali Kolombo amewataka Mamlaka ya bandari na TEMESA kuwa na tabia ya kutoa taarifa mapema wanapoona kuna viashiria vya kutokea kwa changamoto kabla haijatokea kulingana na uzoefu wao kwani wanaoumia zaidi ni abiria (Wananchi) na hivyo kuwataka uzembe huo usijirudie tena.
Hata hivyo Kanali Kolombo ametoa pole na kuomba radhi kwa Wananchi waliokwama bandarini hapo na kuwahakikishia kuwa tayari amekwisha wasiliana na TEMESA na mafuta yapo njiani hivyo baada ya saa chache usafiri utarejea kama kawaida ambapo safari yao ilitarajiwa kuanza saa 8 usiku kulingana na ratiba ya maji kwa sasa lakini pia kutokana na kuharibika kwa Tishari kisiwani mafia.
Akitoa ufafanuzi wa mabadiliko ya safari hiyo Nahodha wa meli Bw. George Charles amesema moja ya sababu za usumbufu uliotokea umetokana na kuharibika kwa tishari (sehemu ya kushukua abiria) katika mji wa mafia kwani kwasasa inawalazimu kutia nanga ufukweni mwa bahari hivyo wanajitahidi safari zao zote zitazingatia ratiba ya kupwa na kujaa kwa maji katika kisiwani mafia.
Aidha wananchi waliokwama katika bandari hiyo wamemshukuru Mhe. Kolombo kwa kusikia kilio chao na kufika kuwaona huku wakisisitiza umakini wa usimamizi wa bandari kuimarishwa zaidi ili kero hiyo isijirudie tena.
Wananchi hao walianza safari hiyo saa 8 usiku kama walivyoahidiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na asubuhi ya leo tarehe 11.09.2024 wakawasili Mafia.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.