Maadhimisho ya wiki ya sheria nchini hufanyika kila mwaka. Lengo la maadhimisho haya ni kutoa Elimu ya kisheria kwa kutumia majukwaa na mikutano mbalimbali ya wananchi ili kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi badala ya kwenda mahakamani ambapo mara nyingi wananchi wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta haki hali inayopelekea kushuka kwa kiwango cha uzalishaji mali.
Kwa mwaka huu wa 2024, madhimisho ya wiki ya Sheria Wilayani Kibiti yamezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mhe. Kanali Joseph Kolombo siku ya Jumamosi tarehe 27 Januari, 2024 kwa kufanya matembezi kutoka katika viwanja vya Mahakama ya wilaya ya Kibiti hadi shule mpya ya sekondari ya Chief Hangaya iliyopo katika Kata ya Kibiti kisha kupanda miti katika shule hiyo.
Maadhimisho ya wiki ya Sheria nchini yameanza tangu januari 24 na yanatarajiwa kutamatika ifikapo januari 30/2024 huku kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni "UMUHIMU WA DHANA YA HAKI KWA USTAWI WA TAIFA : NAFASI YA MAHAKAMA NA WADAU KATIKA KUBORESHA MFUMO JUMUISHI WA HAKI JINAI".
Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Kibiti Mh.Tarsila J. Kisoka alisema, maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi ili kujenga jamii ya watu wanaofahamu sheria za nchi yao na kuzifuata. Hivyo watatumia wiki hii kutoa huduma na Elimu ya sheria katika maeneo yafuatayo, Shule ya msingi Kikale, Shule ya Msingi Kitundu, Shule ya Sekondari Zimbwini na kilele cha maadhimisho hayo itakuwa siku ya Alhamisi Februari 1, 2024 yatakayofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Kibiti kuanzia saa 3:00 Asubuhi.
Wananchi wote mnakaribishwa.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.