Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka wakazi wa Kitembo kuitunza na kuilinda Zahanati ya Kitembo ambayo imejengwa na wananchi Pamoja na Serikali yao.
"Zahanati hii ni yenu, itunzeni, ilindeni ni Mali yenu,a ngalieni isiharibiwe na watu wasio na nia njema".Alisema Kanali Kolombo.
Amesema hayo alipokuwa akizindua rasmi Zahanati ya kitembo ambayo inaanza kutoa huduma za matibabu kuanzia Mei 10/2023.
"Nimezindua rasmi zahanati hii, nami nimepima kuashiria huduma zimeanza kutolewa, wananchi wote wenye changamoto ya afya huduma zinapatikana hapa" alisema Kanali Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo amewapongeza wakazi wa Kitembo kwa kazi nzuri huku akisema zahanati ya kitembo imeanza kwa baraka kwani tayari MSD imeanza kusambaza vifaa tiba na Kwa kitembo tayari vimepokelewa.
Kwa upande wa changamoto ya maji Kanali Kolombo amewaondoa hofu wakazi wa kitembo kwa kuwathibitishia kupata maji safi na salama, kwani mpaka sasa mradi wa maji Mkupuka ambao utasambaza maji kitembo umekwishafanyiwa upembuzi yakinifu kilichobakia ni utekelezaji wakati wowote kuanzia sasa utaanza kutoa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo akiwa katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha anajenga nyumba za matabibu wa zahanati hiyo ili waweze kufanya kazi wakiwa katika mazingira mazuri na jambo litakalofanya kuongeza umakini wa utendaji kazi. Pia ameagiza kupimwa eneo lote la zahanati na kuweka mawe ya msingi Ili kutambua mipaka halisi ya Zahanati.
Aidha Mganga wa Mkuu wa Wilaya Dkt. Elizabeth Oming'o Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji amesema lengo la serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi na kupunguza idadi ya vifo vya watoto na wajawazito huku akisisitiza kwamba, Zahanati hiyo itasaidia kutoa huduma mbalimbali za dharura. Pia Dkt. Oming'o amesema Zahahati hiyo tayari imekwishafunguliwa account ya Benki katika Benki ya NMB na habari njema ni kwamba tayari wameanza kupokea dawa kutoka MSD Kwa ajili ya Zahanati hiyo.
Awali akikaribisha Mkuu wa Wilaya Diwani wa Kata ya Kibiti Mhe. Hamidu Ungando ameishukuru Serikali ya awamu ya 6 kwa kazi zilizofanyika na kipekee amewashukuru wananchi kwa namna walivyojitoa tangu kuanza kwa ujenzi mpaka Leo Jengo limekamilika.
"Ndg wananchi, tumepata Jengo hili, linahitaji usimamizi wa karibu, Wataalam walioletwa shirikianeni nao waweze kutuhudumia vizuri" Alisema Ungando.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.