15.5.2024.
Jumuiya ya Jai Mkoa wa Dar es Salaam inayojishughulisha na masuala ya kijamii imemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kibiti msaada wa takriban nguo 5000 kwaajili ya kuwasitiri waathirika wa mafuriko Wilayani Kibiti ambayo yamedumu kwa miezi 2 Sasa.
Akikabidhi msaada huo Mkuu wa msafara na Kiongozi wa JAI Wilaya ya Kinondoni Ndg. Khamis Mmanga ameitaka jamii kuona kuna umuhimu wa kusaidiana panapotokea majanga kwani hakuna anayetarajia kuyapata kwani huja kwa wakati tusioutegemea pasi na maandalizi.
"Hili ni jambo letu sote, niombe tu jamii kuwa na tabia ya kusaidiana na kufarijiana katika majanga na furaha pia" Alisema Mmanga.
Aidha kupitia ombi la Mkuu wa Wilaya kuhitaji kupatiwa mbegu na vyakula, Bw. Mmanga amesema wamelipokea na wanakwenda kujipanga kuhakikisha mbegu, vyakula na vifaa vingine vinapatikana kwa ajili ya waathirika hao.
Akitoa shukrani kwa msaada alioupokea Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka wadau wengine na Taasisi mbalimbali kuendelea kujitokeza kuwasaidia wanakibiti hususani mbegu za mazao mbalimbali ili waweze kupanda upya kwani maeneo yaliyoathirika bado yana unyevu wa kuweza kustawisha mazao.
Nao Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Bungu wilayani Kibiti pamoja na Viongozi wa vijiji wakiwemo mabalozi wametoa msaada wa unga viroba 20 vyenye ujazo wa kg 5 na sabuni ya unga ya kufulia katoni 2 ikiwa ni sehemu ya kuwashika mkono wahanga wa mafuriko Wilayani humo.
Msaada huo umekabidhiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Bungu Kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo jana tarehe 15 mei 2024 katika viunga vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
"Pokea hiki kidogo tulichopata, ukawafikishie wenzentu walioathiriwa na Mafuriko, tumeguswa na tupo pamoja nao" Alisema.
Vilevile katika msafara huo Mwenyekiti wa Kijiji cha pagae Ndg. Shabani Ally Karuke amesema wameguswa sana na suala la Mafuriko Wilaya ya Kibiti hivyo kwa uchache wao viongozi wa Bungu wameona wawasaidie ndugu zao kwa kilichopatikana.
Naye Mzee wa Kata ya Bungu Ndg Ramadhani Mohamed Mkwaya amesema kwa umoja wao wamejikusanya viongozi wa Chama na Serikali kutoa pole kwa wenzao waliopatwa na Mafuriko.
Baada ya mapokezi, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewashukuru viongozi hao msaada huo akibainisha kwamba mahitaji yaliyopokelewa yatapelekwa kwa walengwa.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.