Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibiti Ndugu Hemed Said Magaro, leo tarehe 24/02/2024 ameendesha kikao na Viongozi wa Vyama vya Siasa kuhusiana na Uchaguzi Mdogo wa Udiwani Kata ya Mlanzi unaotegemewa kufanyika tarehe 20/03/2024.
Jumla ya Viongozi waliohudhuria Kikao hicho ni 8 kutoka vyama vifuatavyo: Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Civic United Front (CUF) pamoja na Chama Cha ACT Wazalendo.
Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho, Viongozi wa Vyama walipata wasaa wa kutambuana, Kupitia ratiba nzima ya zoezi la Uchaguzi Mdogo wa Udiwani na kujadili kwa kina matukio yote ya zoezi la Uchaguzi Mdogo wa Udiwani ikiwemo Utoaji wa Fomu za Uteuzi, Uteuzi wa wagombea, Kampeni za Uchaguzi na Siku ya Uchaguzi.
Akihitimisha kikao hicho Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibiti, amewataka Viongozi wote wa Vyama kudumisha Amani, Utulivu, na kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zinazosimamia masuala ya uendeshaji wa Uchaguzi. Pia amewasisitiza Viongozi wa Vyama vya Siasa kuzingatia Ratiba ya utekelezaji wa zoezi la Uchaguzi Mdogo ili kuwa na Uchaguzi ulio huru, wa haki na wenye kuaminika.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.