Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo Bw. Hemed S. Magaro tarehe 30 June, 2023 amewateua watu sita kuwa wagombea wa udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa Kata ya Mahege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Wagombea hao na vyama vyao kwenye mabano ni pamoja na Bw. Seif Adam Mkokwa (UMD), Bw. Musa Juma Maramuah (UDP), Bw. Sultani Said Mpondi (UPDP), Bw. Mrisho Miraji Jongo (CUF), Bw. Hamada Juma Hingi (CCM) na Bw. Sadick Athumani Mzuzuri (NRA)
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo kwenye kata hiyo zitaanza tarehe 01 hadi 12 Julai, 2023 na uchaguzi utafanyika tarehe 13 Julai, 2023.
Tuligawa fomu kwa vyama 7 kwa mujibu wa sheria mpaka June 30, saa 10 :00 jioni, vyama 6 vimerejesha fomu na vyote kuteuliwa kusimamisha wagombea , hivyo kuanzia tarehe 1 - 12 Julai kampeni zinaanza, wananchi jitokezeni kuchagua viongozi wenu kwa amani na utulivu "Alisema Magaro.
Katika zoezi hilo Msimamizi wa uchaguzi Bw. Hemed Magaro amewaagiza wenyeviti wa vijiji kuitisha mkutano wa halmashauri ya vijiji vyao Ili kuweza kuhamasisha na kuwajulisha wananchi juu ya zoezi la uchaguzi litakalofanyika julai 13 mwaka huu.
Vilevile Magaro amewaagiza watendaji wa Kata, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoa taarifa mapema wanapohisi au wanapopata taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani.
"Zoezi hili ni la kitaifa, macho yote ya nchi yako hapa, watendaji ngazi ya Kata, vijiji na vitongoji mna wajibu mkubwa kuhakikisha mnasimamia vizuri uchaguzi huu kwa kufuata Sheria ,kanuni ,na taratibu za uchaguzi kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na amani ili democrasia izidi kuimarishwa" Alisema Magaro.
Aidha Mkurugenzi Msaidizi wa Habari kutoka Tume ya uchaguzi Bi. Leila Muhaji, amewataka Viongozi wa vijiji katika siku zilizosalia kuhakikisha wanatoa matangazo kupitia njia mbalimbali zitakazoweza kuwafikia na kuwajulisha wananchi kujitokeza kupiga kura kulingana na uzoefu wa mazingira yao.
"Tupo hapa kuhakikisha zoezi la uchaguzi linakamilika kama ilivyokusudiwa, watendaji Kata, wenyeviti wa vijiji na vitongoji tunaomba ushirikiano wenu " Alisema Leila Muhaji.
Hata hivyo Viongozi hao waliainisha njia za matangazo ziltakazotumika kuwafikia wananchi wote kuhusu taarifa ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na njia ya Kigoma (lamgambo), redio, gari la matangazo, na kuitisha kikao cha kamati ya Kijiji katika vijiji vyao kuwaeleza wananchi kuhusu uchaguzi huo.
Mara baada ya majina kubandikwa kwa nyakati tofauti wagombea wa vyama vyote wamewapongeza Tume ya Uchaguzi ,Viongozi wa Wilaya kwa namna walivyowapokea vizuri , kwa jinsi walivyo waelimisha na mwisho zoezi hilo kwenda vizuri bila kasoro yeyote mpaka sasa. Pia wagombea hao wameomba wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha uchaguzi unasimamiwa kwa haki. Hata hivyo wagombea walisema kuwa wapo tayari kutoa ushirikiano na kumuunga mkono atakayechaguliwa kuiongoza Kata ya Mahege.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.