Jana 17 Jan 2024, Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameongoza kikao cha wadau wa Elimu wilayani Kibiti ili kuweka mikakati na kushirikishana mambo mbalimbali yanayoihusu sekta ya Elimu wilayani humo kwa mwaka 2024.
Katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Elimu Msingi na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kibiti kwa nyakati tofauti walieleza mafanikio waliyopata kwa mwaka uliopita 2023, Mipango na mikakati iliyopo kwa mwaka huu 2024 upande wa Halmashauri pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Changamoto kubwa iliyoonekana hasa kipindi hiki cha kufungua shule ambapo wanafunzi wapya wanasajiliwa mashuleni ni upungufu wa madawati upande wa Elimu Msingi na viti na meza kwa upande wa Elimu Sekondari.
Kuhakikisha changamoto hii inaisha wadau hao walitoa ahadi ya michango ya Madawati 40, Meza 50, Viti 70 na fedha Tsh. 750,000 huku wengine wakiahidi kuleta kadri watakavyopata na kuweka azimio la kuendelea kuomba kutoka kwa wadau wengine wasiohudhuria na wale wenye mapenzi mema na mustakabali wa Elimu wilayani Kibiti.
Aidha moja ya mkakati uliowekwa na wadau hao ni kuhakikisha Halmashauri inajenga miundombinu kwaajili ya shule ya sekondari itakayochukua Kidato cha Tano na Sita.
“Upande wa Elimu ya Awali na Msingi tayari tumefanikiwa tuna shule za kutosha, lakini upande wa sekondari hatuna shule hata moja ya ‘Advance’ sijui tunafeli wapi” Alihoji Mjumbe mmoja
Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Hemed Magaro alisema Halmashauri tayari ina mpango na wanatenga bajeti kwaajili ya kufanikisha hilo, moja ya shule ambazo ziko kwenye mpango huo ni shule ya sekondari Dimani.
“Moja ya sifa ya shule za ‘Advance’ ni mabweni, shule zetu nyingi tayari zina madarasa ya kutosha pamoja na maabara lakini hatuna mabweni, tukifanikiwa kupata mabweni na miundombinu mingine saidizi hata sasa tunaweza kuiombea usajili ikawa ‘Advance School’” Alisema Magaro
Kanali kolombo alihitimisha kwa kuwashukuru wadau kwa michango na ahadi zao huku akitoa rai kwa watu wote tuendelee kuichangia Halmashauri yetu hata kama ni Kilo moja ya misumari, tuhakikishe Sekta ya Elimu inafanya vizuri Kibiti na watoto wetu wanapata Elimu stahiki.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.