Wadau wa maendeleo ya elimu wa Wilaya ya Kibiti wamekutana katika ukumbi wa shule ya sekondari kibiti kujadili na kupata mwarobaini wa mapinduzi ya elimu kwa kujitathmini, kujipanga Pamoja na kupata mbinu mbalimbali za kuweza kuinua hali ya ufaulu ndani ya Wilaya .
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya elimu Afisa elimu wa Wilaya Bi. Anna Shitindi alieleza kwamba hali mbaya ya ufaulu kwa watoto wa shule za msingi na sekondari kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa ni changamoto kubwa katika Wilaya ya Kibiti kutokana na ufaulu wa wanafunzi kushuka hali ambayo inachangiwa na watoto kushinda na njaa wawapo shuleni, licha ya Jamii yenyewe kuwa chanzo kikubwa cha tatizo hili .
Hayo yamebainishwa katika siku ya wadau wa maendeleo ya elimu Wilaya ya kibiti ambapo Kaimu Mkuu wa Wilaya Meja Edward Gowele amewataka wadau wa Elimu kuamua kwa vitendo kufanya mapinduzi makubwa ya elimu Wilayani humo.
“sasa ni wakati wa kuamua Kwa nguvu zetu zote kufanya mapinduzi makubwa kwenye Elimu, Elimu ni gharama na hatuwezi kukwepa, Serikali imebeba mzigo wote wa ada mashuleni wanafunzi wanasoma bure, hivyo gharama za chakula lazma sisi tuzibebe”alisema Gowele.
Katika kikao hicho Gowele aliongoza majadiliano ya wadau na kuafikiana maazimio mbalimbali baadhi ya hayo ni :- Suala la uchangiaji chakula mashuleni kuwa endelevu, kuchangia vitendea kazi shuleni, wakati huo huo wamewataka wazazi na Jamii kwa ujumla kuanzisha mashamba ya mazao ya chakula ikiwa ni pamoja na kuanzisha kambi za wanafunzi kwa madarasa ya mitihani.
Vilevile Madiwani wametakiwa kuwa desturi ya kuitisha mikutano ya Wazazi kwenye kata zao, kutoa motisha Kwa Walimu waliofanya vizuri, kujenga mifumo ya nidhamu kwa Walimu sambamba na kushawishi Vyama vya msingi kuwa na azimio la kuchangia kwenye Elimu. Hata hivyo wameazimia kutoa taarifa za takwimu za Wazazi wasiopeleka watoto Shule Ili wachukuliwe hatua, kutoa mafunzo Kwa Walimu kazini huku wakisisitiza Viongozi wa Wilaya kutembelea kata zote na kufanya uhamasishaji kwa wazazi kuhusu masuala ya Elimu na umuhimu wake.
Vilevile mkurugenzi mtendaji wa Wilaya Mohamed Mavura licha yakuzungumzia hali mbaya ya ufaulu amewaagiza Walimu ambao shule zao zina maeneo makubwa kuhakikisha wanalima mazao ya chakula mboga na matunda Ili kuweza kufanikisha upatikanaji wa chakula kilicho bora shuleni.
“sitaki kusikia wala kuona shule hazizalishi chakula wakati kuna ardhi ya kuweza kulima mazao ya chakula” alisema Mavura.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.