MUSA KALAGE , ZANZIBAR MASHOA WAIBUKA KIDEDEA.
23.8.2023.
Chama cha wa wafugaji Mkoa wa Pwani kimeteua na kutambulisha Viongozi wa muda wa wafugaji Wilaya ya Kibiti wakati wakisubiri kufanya uchaguzi Mkuu wa kikatiba, unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Zoezi hilo limefanyika Leo tarehe 23.8.2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ambapo Musa Kalage ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa wafugaji Wilaya ya Kibiti huku Zanzibar Mashoa akiteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
" Viongozi hawa tuliowatewa leo wataongoza nafasi hizi mpaka muda wa uchaguzi wa kikatiba utakapofika ".
Akitaja sifa za kupata uongozi katika Chama Cha wafugaji, Mwenyekiti wa wafugaji Mkoa wa Pwani Ngobere Msamau amesema ili mtu ateuliwe au kuchaguliwa lazima ajue kusoma na kuandika, awe na moyo wa kujitolea, awe kiunganishi kati ya Chama Cha wafugaji na Serikali, kiunganishi wa Wafugaji na wakulima.
Vilevile Ngobere amewataka wafugaji kuanza kubadilika kutoka katika ufugaji wa mazoea kwenda ufugaji wa kisasa huku akiwaelekeza Viongozi walioteuliwa kuendelea na zoezi la utoaji wa elimu kwa wafugaji ili waweze kuendana na mabadiliko kila upande utambue umuhimu wa mwenzake na Mali zake.
" Muyapokee mabadiliko, msifuge kwa mazoea, tuna zoezi la uanzishwaji wa ranchi Wataalam wanaendelea kuliratibu katika baadhi ya vijiji vyenu, lipokeeni tukafuge kisasa zaidi tuachane na maisha ya kuhamahama" .
Hata hivyo Ngobere amezungumzia suala la minada ya mifugo kutofanya kazi na kusema kwamba, uelewa wa pamoja unahitajika ili kupata /kuona namna bora ya kuifungua minada hiyo na kuanza kufanya kazi kwa kushirikiana na wafanyabiashara.
" Hii haikubaliki, mtu afugie kibiti, halafu akauzie chalinze, haikubaliki" Alisema Ngobere.
Aidha Chama cha wafugaji kimetoa zawadi ya vyeti vya utambuzi kwa baadhi ya wafugaji ambao wanasimamia amani, hawajihusishi na migogoro katika vijiji wanavyofugia .
Wafugaji waliopewa zawadi ya cheti utambuzi ni Susa Lago, Yohana Mollel, Mkala Bujiku Ndaki, Kisinza Imel na Daktari wa mifugo Mkoa wa Pwani ( RVO) Ramadhan Mwaiganju kwa kazi nzuri aliyoifanya ya uhamasishaji wa uanzishwaji wa ranchi ndogondogo za kufugia mifugo ulioanza kutekelezwa katika Wilaya ya Kibiti.
Akikabidhi uongozi huo uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 2009 mmoja wa wasisi wa Chama Cha wafugaji aliyekuwa Mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Kibiti na Rufiji Bw. Deusi Ndaki amesema ni wakati wa kupisha na wengine kuongoza Chama yeye anapumzika.
"nimedumu kwa muda mrefu nikiwa kiongozi tangu kuanzishwa kwa Chama hiki, nachukua nafasi hii kujihudhulu kupisha wengine nao wachaguliwe kuongoza chama.
Nao baadhi ya wafugaji waliohudhuria kikao hicho, wameomba kuimarishiwa minada kwani changamoto kubwa inayowakabili ni kukosekana kwa masoko kwani wao wanaamini katika chama chao Usimamizi ukiwa imara kila kitu kitakwenda sawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewapongeza wafugaji kwa kuteuwa Viongozi wa muda wakati wakisubiri uchaguzi huku akiamini kuwa wanakwenda kuwa kiunganishi kizuri kati ya wafugaji, wakulima na Serikali.
"Kumekuwa na malalamiko mengi yanayowakabili wafugaji, na haya yanatokana na kutokuwa na mfumo wa pamoja ikiwa ni pamoja na kutohudhuria vikao, badilikeni" Alisema Kanali Kolombo.
" Ili kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima Serikali imekuja na mpango wa uanzishwaji wa Ranchi ndogondogo, na zoezi hili linaendelea kwa sasa katika Kata ya Mtunda kwa sasa baada na kuanza na Kata ya mjawa hatutaki kusikia migogoro lipokeeni".Alisema Kanali Kolombo.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw.Hemed Magaro akasema ngazi ya Wilaya imejipanga kuweka mikakati ya kukuza masoko ya mifugo na malisho ndani ya Wilaya. Pia amewasisisitiza wafugaji kushirikiana kikamilifu kuhakikisha minada ya mifugo iliyopo Wilaya ya Kibiti inafanya kazi na kuongeza mapato ya Halmashauri yanayopotea mara kwa mara.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.