Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg Hemed Magaro leo tarehe 1.3.2024 amefungua mafunzo ya siku mbili ya walimu kazini katika shule zote za wilaya ya Kibiti. Semina hiyo inaendeshwa katika vituo vinne ambavyo ni shule ya Msingi Kitundu, Ruaruke, Bungu na Jaribu Mipakani.
Mafunzo hayo yamehusisha walimu 4 kutoka katika kila shule yaani Walimu 2 wa kiingereza na Walimu 2 wa Sayansi, ambapo zoezi hilo leo linatekelezwa nchi nzima isipokuwa Mikoa 3 ambayo imeshapatiwa mafunzo hayo.
Akimkaribisha Mgeni rasmi Mwezeshaji wa Mafunzo katika kituo cha Kitundu TRC Mwl. Shukuru Mgovano amesema baada ya kuonekana uwepo wa pengo kubwa la vitamkwa sahihi vya herufi katika lugha mawasiliano kwenye somo la kiingereza pamoja na lugha ya komputa inayohusiana na hatua sahihi za utendaji katika somo la Sayansi kwa wanafunzi wengi, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeona ni vema kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa masomo hayo ili waweze kuwaandaa wanafunzi katika misingi iliyobora kwa manufaa ya baadaye.
"Mafunzo yamejikita kwenye mada 2 kwanza (phonological) utamkwaji sahihi wa herufi kwenye lugha ya kiingereza katika lugha mawasiliano (communicative language) ili mwanafuzi wa darasa la 1- 3 wawe na maamshi sahihi. pili mwanafunzi aweze kuwasiliana kwa usahihi kwenye lugha ya komputa inayohusiana na hatua sahihi za utendaji katika somo la Sayansi yaani (coding)" Alisema Mgovano.
Kabla ya Mkurugenzi kuzungumza na Wanasemina, Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi Mwl Zakayo Mlenduka alisema Serikali imeamua kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea walimu uwezo wa kawaida ili waweze kutekeleza mtaala mpya ulioboresha na kujikita kwenye umahiri zaidi.
"Mafunzo yamejikita kwenye umahiri zaidi ili wanafunzi watakapohitimu wapate kuwa na uelewa wa elimu itakayowasaidia kupambana na mazingira" Alisema Mlenduka.
Mwl. Mlenduka amesema wanatarajia baada ya mafunzo hayo watoto wa darasa la tatu wataweza kujieleza kwa lugha ya kiingereza bila hofu jambo litakalowasaidia kwenye soko la ajira pindi watakapohitimu masomo yao kwani watakuwa na uwezo wa kuandika, kusikiliza, kutambua na kujieleza.
Hata hivyo Mlenduka amesisitiza kuwa katika ulimwengu huu wa Sayansi na teknolojia kwa upande wa somo la Sayansi wanafunzi wametakiwa kuanza kujifunza mapema vitu mbalimbali kama vile coding, ili watakapohitimu waweze kuwa na ujuzi utakaowasaidia.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg Hemed Magaro ameipongeza Serikali kwa kuendesha mafunzo kwa walimu katika masomo ya Sayansi na kiingereza kwa kuzingatia umuhimu wake katika Dunia ya sasa.
"Serikali yetu inatoa fedha nyingi kwa ajili ya maboresho ya elimu, na tunaendelea kupokea fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu mbalimbali bila kusahau walimu na wanafunzi na ndiyo maana leo mko hapa" Alisema Magaro.
Mkurugenzi huyo amewasisitiza walimu kuhakikisha wanasikiliza kwa umakini mkubwa yale wanayofundishwa ili watakaporudi katika vituo vyao kazi wakaweze kuwasaidia watoto na walimu wenzao ambao hawakubahatika kushiriki mafunzo hayo.
Magaro aliendelea kusema kuwa, mafunzo hayo yakifundishwa vizuri na watoto kuelewa katika umri huo mdogo yatawajengea msingi imara wa Elimu na kuongeza ufaulu katika masomo yao.
Aidha, kutokana na changamoto ya ufaulu kusuasusa katika Wilaya ya Kibiti, amewapongeza walimu wote kwa juhudi walizozionyesha kwa kipindi kifupi kwani ufaulu umeongeza. Akielezea mafanikio hayo Mkurugenzi Magaro amesema kwa Wilaya ya Kibiti pekee kitakwimu ufaulu umeongezeka kuanzia darasa la 4, 7, kidato cha pili na kitado cha 4.
Baada ya pongezi hizo Magaro amewataka walimu wote kuongeza bidii katika ufundishaji ili Kibiti iendelee kusonga mbele na kuleta Mapinduzi kwenye sekta ya Elimu.
"Walimu mimi niko pamoja nanyi, kwa jambo lolote ambalo naweza kumudu nitalitatua kwa wakati, naomba mnisaidie kuongeza kuufaulu mashuleni najua hilo linawezekana " Alisema Magaro.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.