21.3.2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefungua mafunzo muhimu ya wanajamii wa vijiji 19 vilivyopo karibu na hifadhi ya delta ya mto Rufiji yenye lengo la kuwajengea uwezo na kushirikiana na Serikali kuhifadhi mikoko kwa njia ya Matumizi ya Mtandao wa Kijiografia ujulikanao kama Global Mangrove Watch(GMW).
Akifungua mafunzo hayo Kanali Kolombo amewaagiza Wanajamii hao kusikiliza na kuelewa vizuri watakayofundishwa ili baada ya mafunzo wakaweze kufanya kazi kwa vitendo na weledi mkubwa.
"Nendeni mkatumie vyema mtakachopewa kupitia mafunzo haya kwa vitendo ili mkaimarishe ulinzi na Matumizi endelevu ya Mikoko iliyoko karibu na Vijiji vyenu" Alisema Kanali Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo amewapongeza wakazi wa Delta kwa namna wanavyoishi kwani pamoja idadi ya watu kuongezeka na kupelekea mahitaji ya Wanajamii kuongezeka pia lakini bado Rasilimali za Mikoko zimeendelea kuwepo na kuhifadhiwa.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa nadharia jana 21.3.2024 katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti yakiendeshwa na Mkufunzi Afisa Tehama Ndg. Kuto Edmund kutoka Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki ya Shirika la Wetland International la Mjini Nairobi.
Hata hivyo mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mhifadhi Mkuu Frank Sima kutoka TFS Makao Makuu alifafanua kuwa Wanajamii hao watapewa vishikwambi ambavyo vitasaidia upashanaji wa Habari baina ya TFS na Wanajamii kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002 kifungu cha 99 ambayo inaeleza kuwa, taarifa zitakazotolewa zitakuwa sahihi kwa kuwa zinaonekana kwa njia ya Mfumo wa Kijiografia.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Misitu wa Wilaya ya Kibiti Ndg, Davis Mlowe alisema kuwa TFS inaendelea na itaendelea kushirikiana na Serikali za vijiji kupitia Kamati za Maliasili za vijiji vyote ndani ya Wilaya hususani katika upande wa Misitu ya Mikoko na Misitu ya Nchi kavu pia.
Aidha, Afisa Mradi wa Shirika la Uhifadhi Ardhi-oevu Ulimwenguni Upande wa Tanzania Frank Napoleon katika mafunzo hayo, amekabidhi vishikwambi 11 kwa Wanajamii hao ambao ni Wenyeviti na Makatibu wa Kamati za Maliasili za vijiji 19 vilivyoko karibu na Hifadhi ya Mikoko.
Mara baada ya kukabidhi vishikwambi hivyo Afisa mradi Ndg. Napoleon alisema vifaa hivyo ni sehemu ya Utekelezaji wa randama ya Ushirikiano baina ya TFS na Shirika hilo ambapo tarehe 11.3.2024 walikabidhi ndege 2 zisizokuwa na rubani (drones) na kishikwambi kimoja kwa TFS.
Shirika la Uhifadhi Ardhi-Oevu Ulimwenguni (Wetlands International) linatekeleza miradi mbalimbali inayoendelea kwenye mikoko nchini Tanzania, Kenya pamoja Ethiopia kupitia Mradi ujulikanao kama "Source to Sea".
Mara baada ya kupatiwa mafunzo, Wenyeviti na Makatibu wa Kamati za Maliasili za vijiji wamesema kupitia mafunzo hayo wataongeza weledi wa utendaji kazi na kupata taarifa zilizo sahihi kwa wakati. Vilevile Wanasemina hao, wamelipongeza shirika la Wetland International kwa kuandaa mafunzo na kutoa vishkwambi huku wakisema vitawasaidia kupata taarifa nyingi zaidi kwa muda mfupi zikiwa sahihi.
Mafunzo hayo yametamatishwa kwa kufanya mazoezi kwa vitendo katika Kijiji cha Nyamisati ambapo simu janja hizo (vishkwambi) ziliunganishwa na Mfumo kuweza kutambua baadhi ya maeneo yenye uharibifu ndani ya msitu wa mikoko.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.