Wanajamii wa Wilaya za Kibiti, Mkuranga Kisarawe, Rufiji na Bagamoyo Mkoa wa Pwani kwa uwakilishi wa vikundi vyao wamepatiwa mafunzo ya siku 2 ya ufugaji wa nyuki yaliyofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Kibiti ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuhifadhi Mazingira.
Mafunzo yamelenga kutoa uelewa wa pamoja juu ya mazao ya nyuki, kuwaandaa Wanavikundi vya ufugaji nyuki kuwa wahifadhi wakuu wa mazingira katika maeneo yao. Pia yamelenga kuelimisha namna bora ya kuzalisha mazao mengi na safi ya nyuki kwa kutumia rasilimali ya misitu iliyopo vijijini sambamba na kujipatia ajira ambayo itawawezesha kupata kipato na kujikimu kiuchumi.
Washiriki hao wamefundishwa kutambua namna na sababu ya kuanza ufugaji, mazao ya nyuki, manaeneo yanayostahili kuweka mizinga (manzuki) aina ya nyuki, faida za mazao ya nyuki n.k.
Licha ya kupewa uelewa wa pamoja washiriki hao wamefanya mafunzo kwa vitendo ambapo wamefundishwa kutambua maadui wanaofukuza nyuki kwenye mizinga na namna ya kuidhibiti, kutengeneza vianzio vya masega, namna ya kutundika mizinga na namna ya kutumia vifaa mbalimbali vya nyuki kama vile mavazi ya kujikinga, mashine ya kukamua na kupakia asali
Washiriki hao wamesema wamefarijika sana kupata mafunzo kwani yamewapatia uelewa wa pamoja kwa kubadilishana mawazo na kutengeneza uwanda mkubwa zaidi wa ufugaji nyuki. Vilevile wamesema wanatarajia vikundi vilivyopo kuanza kufanya kazi baada ya kujua namna ya kutumia mizinga huku wakihamasishana kuungana kwa pamoja kuweza kuwa na ufugaji nyuki wenye tija Mkoa wa Pwani.
Awali Mtathimini na Mfuatiliani wa shughuli za mradi huo Bi. Donata Didas aliwataka washiriki wote kuwa wasikivu kwani mafunzo hayo yatawajengea uelewa wa pamoja, huku akitarajia kuwa wanakwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kutoa elimu katika maeneo wanayotoka wakiwa wakufunzi Wakuu.
Aidha, Mratibu wa mradi huo Wilaya ya Kibiti Ndg, Dotto Mandago amesema mafunzo hayo yatasaidia kukuza tasnia ya ufugaji nyuki kuwa endelevu na tayari kwa Kibiti wamekwishapokea mizinga 10 ya kuanzia kazi. Pia amewasitiza washiriki wote kwenda kuwa walimu wazuri kwa wanajamii ambao hawakupata bahati ya kushiriki.
TaTEDO-SESO ni Taasisi ya kiraia ya inayoendeleza huduma ya nishati endelevu yenye lengo la kuboresha maisha ya jamii kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati endelevu kwa kupitia mradi Jumuishi wa kuhifadhi Misitu na kuboresha mnyororo wa thamani wa mkaa unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya waliowezesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Fedha
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.