Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka wananchi kuacha tabia ya kuondoa mashauri mahakamani na kuyarudisha majumbani kwa madai kwamba watamaliza nyumbani kwani ni chanzo kikuu cha kupoteza haki hususani kwenye masuala ya ukatili wa kijinsia.
"Acheni sheria ifuate mkondo wake , hii tabia ya kudai tutamalizana nyumbani inasababisha matukio kuendelea kuongezeka" Alisema Kolombo.
Kanali Kolombo ameyasema hayo katika kilele cha wiki ya sheria yaliyoanza januari 27 na kuhitimishwa leo Februari mosi katika Ofisi za Mahakama ya Wilaya ya Kibiti.
Akizungumzia kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo " Umuhimu wa haki kwa ustawi wa Taifa, nafasi ya wadau katika kuboresha mifumo jumuishi ya haki jinai" Kanali Kolombo amewataka watumishi wote wa Idara ya Mahakama kutenda haki kwa wananchi wanaowatumikia sambamba na kuwapa elimu ya sheria.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wafanyakazi wa Idara hiyo, kufanya kazi kwa bidii ili waweze kumaliza kwa wakati mashauri ya kesi mbalimbali zinazofikishwa mahakamani hapo kutokana na msongamano wa kesi mahakani.
"Nimesikia kuna jumla ya mashauri 189 mahakamani bila kuwa na juhudi hamuwezi kuyamaliza kwa wakati, fanyeni kazi kwa bidii". Alisema Kolombo.
Hata hivyo Kanali Kolombo amewasisitiza wadau hao wa mahakama kuhakikisha wanaelewa vizuri mfumo wa matumizi ya tehama kwani utarahisisha na kukamilisha kazi kwa muda mfupi na haraka zaidi.
"Mnakwenda kuanza kutumia mfumo wa tehama katika utendaji wenu, ninawasihi mkajifunze na kuelewa vizuri kwasababu mfumo utakwenda kuwarahisishia kumaliza kazi kwa wakati,katika ulimwengu wa Sasa wa Sayansi na Teknolojia " Alisema Kolombo.
Aidha Hakimu wa Wilaya ya Kibiti Mhe. Tarsila John Kisoka amemshukuru Mkuu wa Wilaya, Viongozi wa Chama na Serikali, Taasisi mbalimbali na Viongozi wa Dini kwa kushiriki kufunga maadhimisho hayo muhimu ya sheria ambayo hufanyika kila mwaka Duniani.
"Ninawashukuru Viongozi wote kwa ushiriki wenu, maadhimisho haya hutambulika Duniani kote na ni ishara kuu kwamba, mahakama za Tanzania zinatimiza wajibu wake kwa kutenda haki bila ubaguzi" Alisema Mhe. Kisoka.
Naye Afisa Utumishi wa mahakama hiyo Bw. Shadrack Mlomo amewashukuru Waheshimiwa Mawakili wote kwa namna walivyotoa elimu ya Sheria kwa wananchi, huku akiahidi kwamba wataendelea kutoa haki kwa weledi mkubwa, uadilifu na uwajibikaji kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu za Mahakama nchini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.