Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti wamepewa mafunzo ya mfumo wa uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha (FFARS) wanaotakiwa kuutumia tangu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha 2023/2024.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Sudi S. Khassim alisema FFARS ni mfumo wa uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha kwa ngazi ya kutokea huduma kama vile shule, Zahanati, vituo vya afya na Sasa unaanza kutumia katika ngazi ya vijiji na Kata. Mfumo huu unalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika nyanja zote za kazi za kifedha zinazofanywa, utunzaji wa rasilimali sambamba na utoaji bora wa huduma katika Taasisi husika unayoihudumia.
Akitoa mafunzo hayo Mwezeshaji Christopher Bainga amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi, kuhakikisha fedha zinathibitishwa na kutumika vema kwa malengo yaliyokusudiwa.
" Msiogope mfumo, upokeeni utatusaidia, tuupende Ili tuuelewe vizuri ndiyo mfumo unaitumika sasa" Alisema Bainga.
Vilevile amesema, mfumo wa FFARS utasaidia kutoa picha kamili ya kiasi cha fedha kilichopokelewa, chanzo Cha fedha na namna fedha hizo zilivyotumika/ zitakavyotumika.
" FFARS imejikita kufanya manunuzi, kutoa taarifa juu ya fedha zinazoingia, utunzaji na namna fedha zinatumika" Alisema Bainga.
Hata hivyo Bainga amesema, mfumo huo utasaidia kuhakikisha sheria za manunuzi zinafuatwa hivyo ngazi ya Halmashauri na Kata zitakuwa na taarifa sahihi za mapato na matumizi ya fedha.
Mwezeshaji Bainga anefafanua kuwa,Ili kuweza kuingia na kutumia mfumo, Afisa Tehama wa Halmashauri atatengeneza akaunti ya FFARS ambayo itamwezesha mtumiaji kuingia kwenye mtandao huo Kwa kufuata maelekezo ya matumizi ya mfumo.
Naye Afisa Tehama Nasolua Shilla ametoa angalizo kwa watendaji kuhakikisha wanatumia wenyewe mifumo na siyo kwenda kufanyiwa kazi kwani kazi wanazofanya ni za serikali zinahitaji usiri mkubwa.
" Msikwepe kutumia mifumo, tumieni wenyewe na Wala siyo kufanyia kazi steshenari kwani hizo ni nyaraka za serikali" Alisema Afisa Tehama.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Utumishi Sudi S. Khassim amewataka watendaji hao kutumia mafunzo hayo kwa weledi kwa kufanya mazoezi zaidi ili kuelewa mfumo kwa haraka,
"Mfumo huu ni wa kidigitali, ili kuelewa kwa haraka Kila Mtendaji ahakikishe anafanya mazoezi ya mara kwa mara kwa kupitia simu janja mlizonazo" Alisema Sudi
Pia Ndugu Sudi amewaelekeza watendaji wote kuhakikisha wanajaza fomu na wanasajiliwa katika mfumo na kisha watapewa vitabu vya check vitakavyo wawezesha kufanya malipo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.