Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kibiti Ndg. Hemed Magaro amepokea taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za kamati ya lishe wilaya ya Kibiti kwa robo ya nne (Aprili- Juni) ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Taarifa hiyo imetolewa kwenye kikao cha kamati hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Julai 26, 2024. Taarifa zilizowasilishwa kwenye kikao hicho ni kutoka Kitengo cha lishe Wilaya, Idara ya Elimu Msingi, Idara ya Elimu Sekondari, Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Idara ya Maendeleo ya jamii na Kitengo cha kunusuru kaya masikini (TASAF).
Mkurugenzi Magaro amepongeza jitihada za kamati hiyo kwani wamefanya kazi kubwa ya kutoa Elimu ya lishe kwa jamii yote ya Kibiti kupitia vikao mbalimbali, kuwapima hali zao za lishe pamoja na kutoa matibabu ya lishe kwa waliobainika kuwa na utapiamlo mkali na wote wanaendelea vyema.
Aidha Magaro ameitaka kamati hiyo kuwatambua wote wanaosimamia vizuri utoaji wa lishe kama vile shule zinazotoa chakula kwa wanafunzi kwa 100% kupewa pongezi, huku akiwataka na wale wasiosimamia vizuri kutoa sababu za kutofanya vizuri kwenye maeneo yao.
Akifunga kikao hicho Ndg. Magaro ameomba kitengo cha lishe kuwa na utaratibu wa kupima hali za lishe za watumishi wa Kibiti pia.
“Afisa lishe nikuombe usiishie tu kupima watoto na watu wazima huko vijijini, panga ratiba uje utupime na sisi watumishi tuliopo maofisini na kutupa ushauri wa namna gani tunaweza kuboresha hali zetu za lishe” Alisema Magaro.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.