11/3/2023.
Chama cha skauti Wilayani Kibiti kimeadhimisha miaka 106 ya kuanzishwa kwa skauti Tanzania bara, katika viunga vya shule ya Sekondari Zimbwini na kuhudhuriwa na makundi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi na Sekondari.
Skauti Tanzania ilianzishwa tarehe 22/2/1917(Tanganyika) ikitokea Zanzibar ambako ilianzishwa mwaka 1912.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya kaimu Katibu tawala Bw. Lucas Magai amesema, ili kukuza vijana wenye maadili watakao iendeleza nchi baadaye, kuna kila sababu ya kuwa na mafunzo ya skauti katika shule zote ndani ya wilaya hususani vijana wanaoishi maeneo delta.
“Mkawe na mafunzo ya skauti katika shule zote Wilaya ya Kibiti, yatakayosaidia kulea vijana katika maadili mema, uzalendo na kujitegemea ili kujenga Taifa imara.” Alisema Magai.
Magai aliendelea kusema kuwa, uwepo wa makundi ya skauti yanayopata mafunzo na kuyaishi kama skauti ilivyokusudia ni muhimu sana katika ulimwengu wa leo kwani ni dhahiri kuwa tutatengeneza vijana waadilifu wanaojua wajibu wao kwa Mungu, Nchi na wao binafsi kama ilivyo katika kiapo cha skauti nchini.
Vilevile kutokana na changamoto zilizobainishwa katika risala ya wanafunzi na Kamishna wa skauti, Magai amesema amezipokea na atazifikisha mahala husika ili ziweze kutatuliwa huku akiwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao, kwani elimu ni ufunguo wa Maisha yao .
Aidha Kamishna wa skauti wilaya ya Kibiti ndg. Dotto Mandago amesema, lengo la kuanzishwa kwa skauti duniani na nchini kwetu ni kuwafundisha vijana uzalendo, kuipenda nchi yao kuwafundisha vijana stadi za kazi za maisha ya kujitegemea, kuwaheshimu Viongozi wao na kuja kuwa Viongozi bora baadaye. Pia Kamishna Dotto aliendelea kusema kuwa, skauti hufundisha vijana namna ya kuona umuhimu wa kuilinda nchi yao, kutunza rasilimali zilizopo na kuwafanya vijana kuwa wakakamavu ambapo watakuwa tayari kutetea maslahi ya umma muda wowote.
Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi Shakira Sume amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia chama cha skauti nchini, katika ngazi ya Wilaya wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa jamii kuhusu kuitambua skauti, kutopata mafunzo ya uokoaji, ukosefu wa ofisi rasmi ya Kamishna, ukosefu wa vifaa vya michezo mbalimbali, ukosefu wa maeneo ya kufanyia miradi mashuleni na baadhi ya wazazi kushindwa kumudu gharama za Kambi Kwa watoto wao.
Aidha katika risala hiyo wanafunzi wamemwomba mlezi wa skauti, kuwasaidia kujenga ofisi ya kamishna wa skauti wilayani, wameomba kutafutiwa wataalamu wa skauti Kwa ajili ya kuwajengea uwezo n.k.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.