Tarehe 23.5.2024, Taasisi za WIPAHS na KHOJA SHIA ITHNAASHARIA kwa umoja wao wamekabidhi msaada wa kibinadamu kwa ajili ya waathirika wa Mafuriko Wilayani Kibiti.
Akikabidhi msaada huo Muasisi wa Taasisi ya KAPHAS Ndg. Haji Saheeb ametoa pole nyingi kwa waliokumbwa na Mafuriko huku akibainisha kuwa misaada wanayoikabidhi ni sehemu ya michango ya waumini na shule ya WIPAHS.
Baada ya kupokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Denis Kitali amezishukuru Taasisi hizo kwa misaada waliyoitoa akisema, msaada huo utawasaidia watoto ambao wameathiriwa na mafuriko na sasa wamewekwa kambini katika Shule ya Msingi Kitundu wakiwa kwenye maandalizi ya mitihani.
Aidha Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi Mwl Zakayo Mlenduka amesema msaada huo umefika wakati muafaka kwa Vijana hao waliowekwa kambi shuleni hapo baada ya shule zao kufungwa kutokana na kuzingirwa na maji ya Mafuriko, shule hizo ni Beta, Muyuyu, Nyambele na Motomoto.
"Tunawashukuru kwa misaada hii, tuliona ni vema kuwaweka Kambini watoto hawa wa darasa la 4 na la 7 ili waendelee kusoma na kujiandaa kwa mitihani yao ya Taifa.
Naye mratibu wa maafa Wilaya ya Kibiti Ndg. Zakayo Gideon akatoa shukrani za dhati kwa wadau hao huku akibainisha kuwa wamepokea vifaa mbalimbali kama vile magodoro 20, ndoo ndogo za kunawia 25, shajala na vifaa vya shule, vyombo vya kulia chakula na ahadi ya magodoro 80.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.